Lydia Lugakila, Misenyi.
Malunde 1 blog imefunga safari hadi shule ya Sekondari Bugandika ili kubaini chanzo cha wanafunzi wa kidato cha pili kutofanya vizuri katika mtihani wa Taifa 2024/2025 ambapo baadhi ya walimu na wanafunzi wamedai wazazi walezi na jamii kwa ujumla imekuwa chanzo cha kufeli kwao kama ambavyo alibainisha Mwalimu wa taaluma Michael Kedmon.
"Matokeo hayakifichi kwakweli hatukufanya vizuri hasa kwa mtihani wa kidato cha pili Ila hatufi moyo, tutaweka vizuri mipango kwa mwaka 2025 pia tumebaini asilimia 50 ya Wazazi hawana mwamko ni wachache wanaelewa na kuchangia mahitaji ya shule hasa wamezorota sana hawachangii ipasavyo katika suala la lishe kwa watoto na ni ngumu mtoto kusoma akiwa na njaa" alisema Michael
Ameongeza kuwa walimu walishatoa semina kwa wazazi juu ya changamoto ya mtoto kusoma akiwa na njaa na tayari na wameweka mikakati mizuri ya kupokea chakula, kukitunza na kukitumia kama lishe shuleni.
Michael aliongeza kuwa jumla ya wanafunzi hao wa kidato cha pili walikuwa ni 148 waliofaulu walikuwa 105 na waliofeli ni 50.
Alisema kuwa kwa mwaka 2024 walikuwa na jumla ya wanafunzi 548 kwa shule nzima ambapo wazazi waliokuwa wakichangia lishe walikuwa ni 253 Hadi 300 jambo lililoleta ugumu ambapo kwa sasa wamekubaliana na wazazi kuwa watakao sua sua kuchagia lishe watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Mwalimu huyo amesema Wazazi wamekuwa hawashirikiani vyema na walimu katika baadhi ya maamuzi ikiwemo vikao vya shule, mwitikio mbaya katika kukagua maendeleo ya watoto wao, kutochangia baadhi ya michango inapohitajika, kuzorota katika masuala ya uchangiaji lishe shuleni, umbali mrefu wa wanafunzi kufuata huduma ya elimu.
Walimu hao wametaja kupokea matokea hayo kwa masikitiko makubwa na kueleza kuwa imeleta taswira mbaya katika shule hiyo huku wakijipanga upya na kuwa hali hiyo haikubariki na haitajitokeza tena.
Mwalimu huyo wa taaluma alisema kuwa mbali na wazazi kuwa na mwamko mdogo katika kuchangia masuala ya shule pia wamekuwa wakikumbana na changamoto mbali mbali ikiwemo maabara zilizopo kutoridhisha zimejengwa muda mrefu jambo linalosababisha baadhi ya mifumo kuharibika, ukosefu wa nyumba za walimu, ukosefu wa bweni kwa watoto wakike na kiume, ukosefu wa walimu wa sayansi.
Kwa upande wake Mkuu wa shule Msaidizi Obadia Athanas amesema wanajipanga kupambana na changamoto zilizopelekea matokeo mabaya kwa kidato cha pili licha ya Wazazi na walezi kuwa wazito sana na watajitahidi kuimarisha mawasiliano ya mara kwa mara na wazazi ili wawafuatilie watoto wao, kuitisha vikao kila mara.
Aidha Athanas aliongeza kuwa ni wakati sasa Wazazi kujenga tabia ya kushiriki katika mipango na maamuzi ya shule ili kusukuma taaluma mbele.
"kesi ya watoto kutoka umbali mrefu bado ni changamoto tulianzisha mradi wa kuwa na bweni mwitikio wake bado ni mdogo kwa wazazi"alisema Athanas.
Akizungumza mwitikio wa wanafunzi wanaripoti kuanza kidato cha kwanza kuanzia Januari 13 hadi 14 alisema hauridhishi kwani walikuwa wamepokea wanafunzi 28 wakiwa hawajakamilika ki mahitaji huku wakiwa walitegemea kupokea wanafunzi 148.
Hata hivyo Renatus Renard na Grolia Charles ni wanafunzi wa kidato cha nne mwaka 2025 wameiomba Serikali kulipa uzito suala la ujenzi wa bweni kwani wanatembea umbali mrefu wa kilometa 3 hadi 4, kuongezewa walimu wa masomo ya Sayansi na Biashara kwani waliopo ni wachache, walimu wajengewe nyumba za shule kwani hakuna nyumba kabisa tofauti na moja iliyopo na chakavu ya Mkuu wa shule hiyo huku wakiwaomba wazazi kujenga tabia ya kufuatilia Maendeleo yao na kutosubiri waende kuwachukua baada ya kumaliza kidato cha nne.
Social Plugin