Na Marco Maduhu,DODOMA
WAZIRI wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Prof: Palamagamba Kabudi,amekemea tabia ya baadhi ya Watangazaji kuharibu lugha ya Kiswahili 'kubananga" wakati wa utangazaji na kuirisha hadhira taarifa mbalimbali.
Prof. Kabudi amebainisha hayo leo Februari 13,2025 wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji Tanzania ' Annual Broadcasters' Conference' ,ulioenda sambamba na maadhimisho ya siku ya Redio duniani, katika ukumbi wa New Generation Dodoma
Mkutano huo wa siku mbili (Februari 13 na 14,2025) umeandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ukishirikisha Vituo vya utangazaji, waandaaji na wasambazaji wa maudhui mtandaoni, wauzaji wa vifaa vya utangazaji na wadau wote wa sekta ya utangazaji unaongozwa na kauli mbiu 'Wajibu wa vyombo vya utangazaji kuelekea uchaguzi mkuu 2025'.
Amesema sekta ya utangazaji ni muhimu sana katika kuhabarisha umma na hata serikali imekuwa ikitumia vyombo vya habari kufikisha ujumbe wake kwa wananchi, lakini kumekuwa na janga la matumizi ya maneno ya lugha ya Kiswahili ambayo siyo fasaha na sanifu.
"Vyombo vya habari ni muhimu sana na ni kiungo kati ya wananchi na serikali, hivyo mnapotangaza tumieni maneno kwa Kiswahili fasaha na sanifu na siyo "kubananga" mfano kutamka apa badala ya hapa, au uyu badala ya huyu" amesema Prof. Kabudi.
"Acheni kukifubaza Kiswahili, kukidumaza na kukibananga kwa kuyapa maneno ya kawaida ya Kiswahili maana isiyostahili na matokeo yake nchi zingine zimeanza kusema Watanzania ni watumiaji wa lugha ya Kiswahili lakini Kiswahili chao siyo fasaha",ameongeza.
Aidha, amesema kupitia Mkutano huo vyombo vya habari hasa Watangazaji, wanapaswa kusahihisha makosa yao na kutumia Kiswahili fasaha na sanifu pamoja na kuwakumbusha Watanzania hakuna neno uyu bali ni huyu kwa sababu uharibifu huo wa lugha umeenea karibu taifa zima.
Prof. Kabudi ameikumbusha sekta ya vyombo vya habari, hasa redio, kuhakikisha vinatayarisha vipindi vyenye tija vya kuelimisha jamii, ikiwemo namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi huku akionesha wasiwasi kwa maudhui mengi ya vipindi yanavyolenga sana muziki, michezo, na burudani.
Katika hatua nyingine, alizungumzia kauli mbiu ya Mkutano huo, 'Wajibu wa Vyombo vya Utangazaji kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025', na kuwasihi waandishi wa habari kutumia taaluma zao kusimamia haki na usawa katika kuhabarisha umma, huku wakizingatia weledi, sheria, na kanuni za utangazaji.
Alisisitiza pia waandishi wa habari kuepuka habari za kugushi, hasa kwa kuzingatia mabadiliko ya kiteknolojia katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, ili kuepuka kupotosha umma au kuleta taharuki.
Prof. Kabudi ametoa pongezi kwa waandishi wa habari kwa juhudi zao za kuhabarisha umma kuhusu taarifa mbalimbali za serikali, ikiwa ni pamoja na Mkutano Mkuu wa Nishati uliohudhuriwa na Marais kutoka nchi mbalimbali, uliofanyika jijini Dar es Salaam, na akawasihi waendelee kuelimisha wananchi kuhusu jinsi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwani hiyo ni ajenda ya kitaifa.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui, Saida Muki, amesisitiza kuwa waandishi wa habari wanapaswa kuwa makini na matumizi ya Teknolojia ya Akili Bandia (AI) wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu ili wasiwasilishe maudhui yanayoweza kupotosha umma.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Grayson Msigwa, amewashauri waandishi wa habari kuwa, kupitia Mkutano huu, wanapaswa kuzingatia weledi katika taaluma yao hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu ili kulinda usalama wa taifa.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Jabir Bakari, amesema mkutano huu umeandaliwa ili kujadili masuala muhimu yanayohusu sekta ya habari na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazokikabili sekta hiyo.
Akizungumzia Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, Dkt. Bakari amewasihi waandishi wa habari kutumia taaluma zao vizuri, kuhabarisha umma kuhusu hatua zote za uchaguzi hadi siku ya kupiga kura.
Baadhi ya waandishi wa habari wameelezea kuridhishwa na hatua ambazo serikali imekuwa ikichukua katika kuimarisha sekta ya habari.
Social Plugin