

Na Regina Ndumbaro Tunduru.
Wakazi wa Kijiji cha Ligunga, Wilaya ya Tunduru, Mkoa wa Ruvuma, wameanza kupata matumaini ya upatikanaji wa maji safi na salama baada ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuwa katika hatua za mwisho kukamilisha mradi wa kisima kirefu.
Mradi huo unatarajiwa kuhudumia wakazi 4,242 wa kijiji hicho, ukipunguza changamoto ya upatikanaji wa maji ambayo imewakumba kwa muda mrefu.
Baadhi ya wakazi wa Ligunga wamesema ujenzi wa mradi huo umewapa faraja kubwa, hasa kwa akina mama na watoto ambao walilazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji.
Sada Mshamu, mkazi wa kijiji hicho, amesema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutakuwa mkombozi mkubwa kwa wanawake na watoto, kwani muda waliokuwa wakitumia kutafuta maji utaelekezwa kwenye shughuli nyingine za maendeleo.
"Mshamu amesema kuwa Ukosefu wa maji ya uhakika umekuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya kijiji chetu. Tumekuwa tukitumia muda mwingi kuchota maji mtoni au kusubiri kwenye mabomba ya kupampu kwa mkono, hali inayotufanya kushindwa kujikita kwenye shughuli za kujikwamua na umaskini,"amesema.
Yusuf Yasin ni mkazi mwingine wa Ligunga, amesema changamoto ya maji imeathiri maendeleo ya kijiji, kwani muda mwingi unatumika kutafuta maji badala ya shughuli za kiuchumi.
"Tuna mabomba machache ya kupampu yaliyojengwa tangu miaka ya tisini.
Maji yanapatikana kwa shida, na watu wasiokuwa na nguvu wanalazimika kwenda mtoni au kununua maji kwa gharama kubwa ya kati ya Sh.1,000 na 2,000 kwa ndoo ya lita 20," amesema.
Kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Ligunga, Shija Ndeleba, amesema changamoto ya maji imekuwa chanzo cha migogoro ya mara kwa mara kati ya wakazi wa kijiji hicho.
"Viongozi wa kijiji hutumia muda mwingi kusuluhisha migogoro ya kugombea maji. Tunaiomba RUWASA ikamilishe haraka ujenzi wa miundombinu ya mradi huu ili wananchi waweze kupata maji kwa urahisi na viongozi tujitume zaidi kwenye shughuli za maendeleo mmoja wa wanakijiji hao aitwae Ndeleba alisema.
Mhandisi wa Maji kutoka ofisi ya Meneja wa RUWASA Wilaya ya Tunduru, Felix Kakele, amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025, RUWASA imepanga kutekeleza programu ya uchimbaji wa visima 10 pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kusambaza maji vijijini, ikiwemo Kijiji cha Ligunga.
"Wilaya ya Tunduru imepata jumla ya visima 10 vitakavyogharimu Shilingi milioni 600. Kati ya hivyo, visima 9 vimechimbwa na viko katika hatua mbalimbali za ukamilishaji, ikiwemo kisima cha Ligunga," amesema.
Amesema gharama za miradi hiyo zinajumuisha uchimbaji wa visima, ujenzi wa vituo vya kuchotea maji, ununuzi wa vifaa vya ujenzi kama matofali, saruji, nondo, mabomba, pamoja na mifumo ya umeme wa jua (Solar Power) kwa ajili ya uendeshaji wa mradi kwa gharama nafuu kwa wananchi.
"Tunaweka mfumo wa umeme jua ili kupunguza gharama za uendeshaji wa miradi hii kwa wananchi. Vifaa vyote vimepatikana na tayari ujenzi unaendelea," ameongeza Kakele.
Serikali imeweka lengo la kufanikisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa asilimia 85 kwa wakazi wa vijijini ifikapo mwaka 2025. Hadi sasa, RUWASA Wilaya ya Tunduru imefikia asilimia 83, na kukamilika kwa miradi hiyo kutachangia kuongeza huduma ya maji kwa asilimia 3.5, hivyo kufikisha asilimia 86.6 ifikapo Desemba mwaka huu.
Mhandisi Kakele ameishukuru Serikali Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia RUWASA Wilaya ya Tunduru fedha za kutekeleza miradi ya maji vijijini, ikiwemo uchimbaji wa visima 10 vinavyoendelea kujengwa katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Ujenzi wa mradi wa maji safi na salama katika Kijiji cha Ligunga unaleta matumaini kwa wakazi wa eneo hilo, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji.
Kukamilika kwa mradi huo kutarahisisha maisha ya wananchi, kupunguza migogoro ya maji, na kuwawezesha kujikita zaidi katika shughuli za maendeleo.
Social Plugin