Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ZOEZI LA UKAGUZI WA HUDUMA ZA OPTOMETRIA LATAKIWA KUWA ENDELEVU KUDHIBITI VISHOKA



Na WAF, TABORA

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Honoratha Rutatinisibwa ameomba zoezi la ukaguzi linalofanywa na Baraza la Optometria  kuwa endelevu ili kuwabaini watu wasio na taaluma ya optometria wanaovamia na kijushugulisha na kazi hiyo.


 Dkt. Honoratha amesema hayo leo Februari 28, 2025 wakati akipokea taarifa ya usimamizi shirikishi kutoka kwa Msajili Baraza la Optometria Bw. Sebastiano Millanzi. 

"Ujio wenu kwetu umekuwa na manufaa makubwa, kwani umetuongezea maarifa na kwa kuwa katika zoezi hili mlikuwa na wataalam wetu, hivyo ni imani yangu watakuwa wamechota maarifa ya kutosha", amesema Dkt. Honoratha. 

Dkt. Honoratha amesema awali walikuwa hawana mwongozo sahihi wa shughuli za optometria, hivyo upatikanaji wa Sheria utawaongezea chachu ya uratibu na ufuatiliaji huku akiwasilisha ombi la kupatiwa nyenzo zaidi ikiwepo Kanuni za Sheria ya Optometria. 

Awali akiwasilisha taarifa ya zoezi kwa mkoa wa Tabora, Msajili wa Baraza Bw. Sebastiano Millanzi alisema wamebaini baadhi ya mapungufu ikiwepo baadhi ya wamiliki wa vituo kubinafsisha huduma za optometria katika vituo vyao pasipo kuzingatia Sheria ya Baraza la  Optometria namba 23 ya mwaka 2007.

"Tumeenda kwenye vituo viwili, tulichobaini watoa huduma wamebinafsisha huduma ambazo kimsingi leseni za usajili wao unaonesha kutakiwa kufanya kazi katika mikoa nje ya mkoa wa Tabora, hivyo tumewashauri washughulikie usajili wa huduma zao ndani ya miezi mitatu kutoka tarehe waliotembelewa" amesema Millanzi 

Kuhusu Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Tabora, Millanzi ameshauri kuimarishwa kwa kitengo hicho ikiwa ni pamoja na kufanya huduma za mkoba ili kuongeza wigo wa huduma kwa jamii.

Bw. Millanzi ametumia fursa hiyo kuwaonya wataalam wa optometria nchini kutoa huduma kwa kuzingatia mipaka ya majukumu yao na kutoa rufaa haraka kwa wagonjwa pindi wanapobaini uhitaji wa kufanya hivyo.

Naye Mratibu wa vituo Binafsi Mkoa wa Tabora Dkt. Nassoro Kaponta, akishukuru kwa niaba ya jopo la mkoa amesema, Usimamizi huo umekuwa na tija na manufaa kwao kwa kuwajengea uwezo na kuanzia sasa wataendelea kufanya ukaguzi wao wenyewe bila kusubiri ngazi ya Taifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com