Na Dotto Kwilasa, Dodoma
TAASISI ya Foundation for Disabilities Hope (FDH) imetoa tuzo kwa Abilis Foundation kwa kutambua juhudi zake muhimu katika kusaidia watu wenye ulemavu katika maeneo ya Global South.
Tuzo hii inatambulika kama ishara ya kutia moyo na kuthibitisha mchango wa shirika hilo katika kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu.
Akizungumza na Matukio Daima kupitia simu, Mratibu wa Abilis, Winniel Manyanga amesema kuwa tuzo hiyo inaonyesha kwamba juhudi zao zimeanza kuzaa matunda katika jamii.
Amefafanua kwamba shirika lao limejikita katika kuleta mabadiliko chanya kwa njia ya elimu, uhamasishaji, na kutoa fursa za kiuchumi kwa watu wenye ulemavu.
"Tunashukuru kwa kutambuliwa na tumepokea tuzo hii kwa furaha Kama Abilis Foundation, tunaahidi kuendelea kushirikiana bega kwa bega na Taasisi ya Foundation for Disabilities Hope, kuhakikisha kwamba jamii ya watu wenye ulemavu inapata haki na usawa. Hii ni hatua muhimu katika kuleta mabadiliko na kuondoa vikwazo vinavyowakabili," amesisitiza Winniel.
Na kuongeza "Tuzo hii ni hatua muhimu katika kuhamasisha shirika hilo kuendelea na kazi yake ya kuimarisha maisha ya watu wenye ulemavu, huku ikionyesha umuhimu wa ushirikiano katika kutafuta suluhu za kimaendeleo," Amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa FDH, Maiko Salali, kabla ya kutoa tuzo hiyo amewashukuru sana Abilis Foundation kwa kufadhili miradi mbalimbali kwa watu wenye ulemavu
"Tuzo hii ni ishara tosha kwa Abilis Foundation kwani kupitia miradi yao jamii ya watu wenye ulemavu wameweza kuwajengea uwezo na uelewa lengo likiwa ni kuwa na jamii jumuishi”amesema
Naye Mjumbe wa Bodi ya Tasisi ya Foundation for Disabilities Hope na Mbunge wa Viti Maalum, Riziki Lulida, ameishukuru Abilis Foundation kwa kuendelea kusaidia taasisi na makundi ya watu wenye ulemavu.
Amesisitiza kuwa msaada wa Abilis umekuwa muhimu katika kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya watu wenye ulemavu, ikiwa ni pamoja na kuongeza fursa za ajira, elimu,uchumi na huduma za afya.
Lulida ameeleza,kuwa ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kufanikisha malengo ya kukuza ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika jamii.
Mjumbe huyo wa Bodi amewahimiza wadau wengine kujitokeza na kutoa msaada wao ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata haki zao na nafasi sawa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Social Plugin