WANANCHI WAHIMIZWA KUTUMIA ANWANI ZA MAKAZI KUBORESHA HUDUMA KWA JAMII




Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Wananchi wametakiwa kujua na kutumia anwani zao za makazi ili kusaidia kuboresha utoaji wa huduma na kuhamasisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Hayo yamesemwa leo, Februari 6, 2025, jijini Dodoma na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa, wakati akifungua maadhimisho ya Wiki ya Anwani za Makazi Kitaifa, yaliyofanyika katika viwanja vya Jakaya Kikwete Convention Centre.

Waziri Silaa amesema kuwa mfumo wa anwani za makazi ni nyenzo muhimu ya kutoa taarifa na miundombinu inayowezesha kutambua mahali halisi pa mtu au kitu. Hii ni muhimu kwa urahisi wa upokeaji na utoaji wa huduma mbalimbali. Ameongeza kuwa serikali, kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kwa kushirikiana na wadau wengine, ikiwemo Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, inaratibu utekelezaji wa mfumo huu wa anwani za makazi nchini.

"Serikali inatamani kuhakikisha kila nyumba, jengo, kiwanja, huduma, ofisi, au biashara ina anwani ya makazi inayoweza kutambuliwa kwa urahisi. Anwani hii inajumuisha namba ya nyumba, jina la barabara au mtaa, na Postikodi," alisema Silaa.

Waziri Silaa pia alieleza kuwa utekelezaji wa mfumo huu ulianza mwaka 2010 na ulilenga kukamilika mwaka 2015, lakini ulipungua kasi na hivyo kuanzishwa kwa operesheni maalumu ya anwani za makazi, iliyozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Februari 8, 2022.

Aidha, Silaa alisisitiza kuwa utekelezaji wa mfumo huu ni endelevu kutokana na mabadiliko ya makazi na huduma zinazohusiana. Kazi ya kukusanya na kuhuisha taarifa za anwani za makazi inaendelea huku jamii ikihimizwa kutumia teknolojia (TEHAMA) ili kuhakikisha mfumo unafanikiwa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. Festo Dugange, akimuwakilisha Waziri Mchengerwa, alisema kuwa OR-TAMISEMI ni wadau muhimu katika utekelezaji wa mfumo huu kupitia watendaji wa kata, vijiji, na mitaa. Watendaji hawa wanawajibika kuhakikisha kuwa miundombinu inakuwepo na taarifa za anwani za makazi zinakusanywa na kuhuishwa.

"Vilevile, tutahakikisha kuwa mafunzo kuhusu mfumo wa anwani za makazi yataendelea kutolewa kwa waratibu wa mikoa na halmashauri kwa njia ya mtandao (online)," alisema Dugange.

Maadhimisho haya ya kwanza ya Wiki ya Anwani za Makazi yanaongozwa na kauli mbiu isemayo: "Tambua na tumia anwani za makazi kurahisisha utoaji na upokeaji wa huduma."

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com