Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAUZA MAJENEZA BUKOBA WAOMBA HESHIMA.... WAIANGUKIA SERIKALI


*Wadai licha ya kulipa Kodi bado heshima ya biashara hiyo haipo.

Na Lydia Lugakila -Bukoba

Baadhi ya wauzaji na watengenezaji wa majeneza Machinjioni  kata ya Bilele Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera wameiomba Serikali kuwatambua hasa katika biashara hiyo ya Majeneza kwani ni Biashara kama zilivyo biashara nyingine huku wakitaja kukosa Uhuru wa kuuza bidhaa hiyo ikiwa ni pamoja na kupokea  vitisho kutoka kwa baadhi ya viongozi wanaodai Biashara hiyo ifichwe ndani.

Wakiongea na Malunde 1 blog wafanyabiashara hao wa Majeneza ambao hawakutaka majina yao yatajwe wamesema kuwa baadhi ya viongozi wamekuwa wakiitenga  Biashara hiyo huku wakiwazuia kuweka Majeneza hayo nje ya Ofisi au maduka yao.

"Tunazuiliwa kuyaweka nje Majeneza  eti yanawatisha watu sisi tunalazimika kuyaweka majeneza hayo nje kutokana na kwamba tunalipa Kodi ya mapato" ,wamesema wafanyabiashara hao.

Wameongeza kuwa katika mikoa mingine ikiwemo  Mkoa wa Mwanza kuna Ofisi takribani  22 au zaidi na maduka na yanayokuwa wazi kwa kuuza na Hospitali iko pale pale wanafanya biashara hiyo kwa uhuru lakini kwa Bukoba wanachukuliwa kawaida ambapo wengi uishia kusema mtaa wa kuuza majeneza ni Machinjioni wanasema wafanyabiashara hao.

Wafanyabiashara hao wamesema kuwa wamechoka kuongelewa vibaya ikiwemo kubezwa na baadhi ya watu wanaodai kuwa wafanyabiashara hao wanapaswa kuiogopa  Biashara ya majeneza huku wakiieleza jamii kuwa hiyo ni biashara kama ilivyo biashara nyinginezo.

"Sio wote tuna uwezo  wa kuendesha pikipiki   hivyo tumejiajiri viongozi watutembelee na kuona fursa zilizopo kwani tunao uwezo wa kuwafundisha vijana maana tunazeeka pia watoto wanaotoka vyuo vya ufundi huogopa hii shughuli", wamesema.

Wakitaja changamoto mbali mbali wanazozipitia wamesema kuwa ni pamoja na ukosefu wa rangi za kupuliza magari ambazo hutumika kupaka majeneza hayo kutopatikana kwa urahisi,umeme kukatika wakati wakiwa na oda za watu jambo linalowakwamisha, pia wateja kudhaminiwa majeneza kisha kutorejesha fedha zao kwa wakati au wakati mwingine kutokomea kabisa.

Aidha wameongeza kuwa wanapata changamoto ya gharama kubwa za mapambo ya Jeneza na baadhi ya vifaa kwani hupatikana Nchini Kenya ambapo wakati mwingine uagizwa kwa njia ya mtandao hadi kufika Mkoani Mwanza ambapo pia huletwa kwa njia ya meli hadi Bukoba.

Hata hivyo wameiomba Serikali kuwaangalia wafanyabiashara hao kwa jicho la tatu ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kupata mikopo ya kuendesha Biashara hiyo huku wakiomba ipewe heshima kwani hawaombi watu wafariki bali ni biashara kama nyingine.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com