Na Dotto Kwilasa, MTWARA
WIZARA ya Katiba na Sheria imehitimisha kambi ya mafunzo na utoaji wa elimu ya uraia na utawala bora mkoani Mtwara kwa viongozi wa ngazi mbalimbali, kuanzia ngazi ya mkoa, wilaya, kata, hadi vijiji sambamba na kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia, iliyokuwa ikitoa huduma kwa wananchi katika halmashauri zote za mkoa huo.
Mafunzo haya yalilenga kuimarisha uelewa wa viongozi na wananchi kuhusu haki na wajibu wao katika utawala bora, sheria, na demokrasia.
Akizungumza na Waandishi wa habari mara baada ya kuhitimisha mafunzo hayo, Wakili wa Serikali Mkuu na Mratibu wa Mafunzo ya Elimu ya Uraia na Utawala Bora kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Prosper Alexander, ameeleza kuwa kwa jumla mafunzo hayo yameendeshwa kwa ufanisi na mafanikio.
Amesema kuwa mafunzo hayo yamefanikiwa kuyafikia makundi yote muhimu, ikiwa ni pamoja na Kamati za Usalama za mkoa, wilaya, na watendaji wa kata na vijiji.
“Tumefanikiwa kufika katika halmashauri zote tisa za wilaya hapa Mtwara. Tumeona wahusika wamefurahia mafunzo haya na wanatamani yawe endelevu. Wameahidi kutumia elimu waliyopata katika utekelezaji wa majukumu yao,” amesema Alexander.
Aidha, amesema matarajio ya Wizara ni kuona matokeo chanya ya mafunzo hayo yakionekana katika jamii, ambapo viongozi na wananchi watakuwa na uelewa bora wa haki zao na utawala bora.
Naye, Wakili wa Serikali na Mratibu Msaidizi wa Mafunzo ya Elimu ya Uraia na Utawala Bora, Rhoda Longwe, amesema mafunzo hayo yamekuwa na tija kubwa kwani washiriki wamependekeza kuwa yafanyike katika mikoa yote nchini.
Longwe amebainisha kuwa mafunzo haya yameongeza ufanisi katika usimamizi wa sheria na utawala bora, hivyo kuweka misingi imara ya maendeleo endelevu katika mkoa wa Mtwara na maeneo jirani.
Naye Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Mwanasheria wa Serikali, Nicholas Edward Mhagama, ameeleza kuwa mada ya ulinzi na usalama ni miongoni mwa mada zilizopewa kipaumbele katika mafunzo hayo, na kwamba mwitikio kutoka kwa washiriki umekuwa mkubwa.
"Baada ya mafunzo haya ni matumaini yangu kuwa kutakuwa na ushirikiano mkubwa baina ya vyombo vya usalama na jamii," amesema Mhagama.
Afisa Utumishi kutoka Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Agness Mabago, amesema kuwa mafunzo hayo yamegusa namna mamlaka kwa Umma inavyofanya kazi, na pia kuhamasisha ushirikishwaji wa wananchi wa chini katika maamuzi ya utawala.
"Mafunzo haya pia yatasaidia wananchi kujua haki na wajibu wao, ikiwa ni pamoja na matumizi sahihi ya sheria zilizowekwa na Serikali katika kufanya maamuzi," ameongeza Mabago.
Kwa upande wake, Afisa Uchunguzi kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Juliana Laurent, amesema kupitia watumishi waliopata mafunzo hayo itasaidia kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki zao za msingi na jinsi ya kuzilinda.
Laurent ameeleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha demokrasia inaimarika na haki za binadamu zinaheshimiwa kwa kiwango cha juu.
Mafunzo haya ya uraia na utawala bora yanaendelea kuwa na mchango mkubwa katika kujenga jamii yenye uelewa wa kisera, kisheria, na kijamii, na kuwa sehemu ya jitihada za Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan za kuimarisha utawala bora na maendeleo endelevu katika mikoa yote ya Tanzania.
Social Plugin