Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WADAU WA HABARI, WAANDISHI WA HABARI ZANZIBAR BADO WANALIA NA SHERIA KANDAMIZI


Na Masanja Mabula -PEMBA

Ni takribani miaka 28 sasa tangu sheria ya Usajili na Uwakala wa Habari, Magezeti na Vitabu No/1988 ambayo ilifanyiwa marekebisho 199 ifanyiwe marekebisho ambayo hata hivyo bado hayajaleta suluhisho la changamoto zinazawakabili waandishi wa habari.

Kwa kipindi chote hicho wadau wa habari wakiwemo waandishi wa habari wamekuwa wakipiga chapuo kuomba sheria ambazo ni kandamizi ziweze kuondoshwa ili kutoa uhuru wa waandishi na wadau wa habari kutumia vyema tasnia hiyo kwa lengo la kuleta mabadiliko chanya.

Kubadilishwa au kufanyia marekebisho sheria kandamizi ikiwemo ile ya Usajili na Uwakala wa Habari, Magezeti na Vitabu No/1988 ambayo ilifanyiwa marekebisho 1997 itatoa fursa na mawanda mapana kwa wadau na waandishi wa habari kutimiza malengo na wajibu wao kwa jamii.

Kifungu cha 30 cha sheria hii kimetoa mamlaka makubwa mno kwa Waziri wa Habari kuweza kuchukua maamuzi ya kukifungia chombo cha habari (Vijarida, vitabu, gazeti) pasi na kuhitaji ushauri kutoka mamlaka nyengine.

Makala haya imefanya mahojiano na baadhi ya waandishi wa habari nguli, weledi na wabobezi katika tasnia ya habari Kisiwani Pemba ambao wametoa maoni yao juu ya sheria hii ambayo wameitaja kuwa ni kikwazo cha maendeleo na uhuru wa waandishi wa habari.

Ali Masoud Kombo Meneja wa Kituo cha Radio Jamii Micheweni amebainisha kwamba Sheria hii siyo tu kuwa ni kandamizi bali pia inaviza maendeleo ya habari nchini.

Katika mahojiano na Makala haya Ali Masoud Kombo anasema mabadiliko ya baadhi ya sheria ikiwemo sheria hii ya Usajili na Uwakala wa Habari, Magezeti na Vitabu No 5 ya 1988 ambayo ilifanyiwa marekebisho na sheria No.8 ya 1997 ili iendane na maendeleo ya tasnia ya habari.

“kwa sasa nilikuwa na mpango wa kuanzisha gazeti na vijarida kwa ajili kuendelea kutoa taarifa kwa umma, lakini nimeshindwa kwani nahofu juu ya sheria hii ambayo imempa waziri mamlaka makubwa ya kuweza kukfungia gazeti”alisisitiza.
Essau Simon Kalukubila mmiliki wa UGA MEDIA ambaye pia ni mwandishi wa habari na mtangazaji wa Radio Jamii Micheweni.

Naye Essau Simon Kalukubila Mmiliki wa UGA MEDIA, amesema sheria hii ni kongwe na ambayo ilitungwa kulingana na mahitaji ya wakati huo,kwa sasa inahitaji kufutwa baadhi ya vifungu ambavyo vinaonekana kuwa ni kandamizi.

“Tangu niingie kwenye tasnia ya habari, waandishi na wadau wa habari wanaendelea kupaza sauti zao kuziomba mamlaka husika kuzifanyia marekebisho baadhi ya sheria ikiwemo hii Usajili na Uwakala wa Habari, Magezeti na Vitabu No/1988 lakini zimeshindwa kufanyiwa marekebisho au sijui hawa wahusika wanainterest nazo”alihoji.

Naye Ali Khatib Chwaya Mwandishi wa Habari Mkongwe Kisiwani Pemba anasema mabadiliko yanahitajika kwani wakati sheria hii inatungwa ilikuwa sahihi kulingana na wakati huo kwa kuwa kulikuwa na vyombo vichache vya habari.

"Nyinyi waandishi wa habari mnaochipukia endeleeni kupaza sauti kuomba hichi kifungu ambacho kinaviza uhuru wa habari kiondoshwe ,jambo ambalo pia litawafanya muwe huru kutekeleza majukumu ya kuihabarisha jamii”alishauri.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye mafunzo ya Sheria ya Habari Mmiliki wa Blog ya Pemba Today Haji Nassor Mohammed amewataka kushirikiana katika kudai marekebisho ya sheria kandamizi zinazobinya uhuru wa waandishi.

Amesema zipo sheria nyingi ambazo zinaonekana kuwa shubiri (chungu) kwa tasnia ya habari ikiwemo hii inayompa mamlaka Waziri wa kufungia na kusitiza utoaji wa huduma (Kuhabarisha) kwa chombo cha habari.

“Mapambano haya tutashinda iwapo kila mmoja kwa kutumia chombo chake ataandika na kutangaza taarifa zinazotaka marekebisho ya sheria hii, itafika wakati wakubali na kuzirekebisha kama sio kuziondoa kabisa.

Mwandishi wa Makala haya binafsi nikiri kwamba mmoja wa wandishi wa habari Kisiwani Pemba ambaye anafaa kuungwa na mkono, ni Haji Nassor Mohammed ambaye amekuwa ni mfano wa kuigwa katika mapambano haya ya marekebisho ya sheria kandamizi.

Kwa upande wake Hawra Shamte, mwandishi wa habari Mkongwe Visiwani hapa, akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari katika Ofisi za Tamwa Pemba alisema kifungu hicho kinampa mamlaka waziri kukifungia chombo cha habari pindi akiona yeye inafaa.

“Kifungu hiki kinahitaji kuondoshwa kwani kinakandamiza uhuru wa habari, kwani ni vigumu kuweza kubaini dhana na shuku, hivyo tunashauri kiondoshwe,” alisema.

Kwa upande wa wadau wa habari kilio chao ni kwa sheria hii kwani wanasema ikiachwa iendelee kutumika inaweza kusababisha umaskini kwa jamii.

Mohammed Suleiman (Babu Eddy) mmiliki wa Rada Online TV, amesema kitendo cha waziri kupewa mamlaka makubwa na sheria ya kuweza kukifungia chombo chochote cha habari kinaweza kuwa ni sababu ya umaskini.

“Vijana wengi wamewekeza kwenye mitandao ya kijamii, hivyo Waziri akiamka na kutoa maamuzi ya kufungia chombo cha habari itachangia umaskini kwani chombo kinategemewa na baadhi ya vijana kuendesha maisha yao,” alisema.

Hata hivyo waandishi na wadau wa habari wameshauri na kutoa mapendekezo yafuatayo;-

Kabla ya waziri kuchukua maamuzi ya kukifungia chombo cha habari , anapaswa kushauriana na wadau wa habari ikiwemo BARAZA LA HABARI TANZANIA –MCT-pamoja na wadau wengine wa habari wakiwemo Vilabu vya waandishi wa habari na TAMWA.

Kuundwe bodi ambayo itakuwa na jukumu la kusimamia na kuratibu mwenendo wa vyombo vya habari.

Wakati umefika kwa watunga sheria kusikiliza kilio cha wadau wa habari na wandishi wa habari cha kutaka kupitishwa sheria mpya ya habari ili waweze kutekeleza wajibu na majukumu yao kwa ufanisi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com