
Na Lydia Lugakila - Kyerwa
Chama cha ushirika cha msingi cha kilimo hai na soko la haki Mkombozi AMCOS wilayani Kyerwa Mkoani Kagera kimeweka mikakati kabambe kwa kipindi cha mwaka 2025/2026 ili kuwainua wakulima wa kahawa pamoja na kuliwekea heshima zaidi zao hilo.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa chama cha Mkombozi Willibard Edward Mugerwa katika mkutano mkuu wa kawaida wa wanachama uliofanyika katika eneo la mradi wa kiwanda cha kukoboa Kahawa kilichopo eneo la Rubwera wilayani Kyerwa Mkoani Kagera uliolenga kupitisha makisio ya mapato na matumizi msimu wa 2025/2026.
Willibard ametaja mikakati mbali mbali kuwa kuwa ni pamoja kutenga mashamba darasa 30 kwa maeneo husika, kuhakikisha wanalipa Wakulima kwa muda muafaka, kutoa motisha kwa wakulima na watendaji watakaofanya vizuri, kuongeza wanachama wapya, kuongeza ajira za kazi, vibarua na watendaji, pamoja na kutafuta kampuni ya ulinzi kwa usalama zaidi wa mali za chama hicho.
Aidha Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa kupitia mikakati hiyo wakulima wa Kahawa wataweza kusonga mbele ki uchumi na kuendeleza heshima ya zao hilo.
Naye Meneja wa Mkombozi AMCOS Alphonce Vedasto kupitia taarifa yake kwa wanachama amesema chama hicho kimepitisha makisio ya bajeti ya mwaka 2025/2026 ya shilingi Bilioni 25.25 na kutangaza bei ya Kahawa kuanzia kununulia kahawa kuwa ni shilingi 6,500 kwa kilo.
Kupitia kikao hicho wanachama hao wamepewa muda wa kutoa maoni kuhusu chama chao na kuhoji masuala mbali mbali ambayo yamepatiwa majibu.
Hata hivyo Mkaguzi Coasco Mkoa wa Kagera Michael Kileo katika taarifa yake amesema mwaka huu chama cha Mkombozi kimepata hati inayoridhisha baada ya ukaguzi wa kuridhisha kuhusu taarifa za kifedha ambazo ziko sahihi.
Social Plugin