TASAF YAFANIKIWA KUSAIDIA KAYA MASKINI NA WATOTO KUSOMA HADI VYUO VIKUU


Mratibu wa Malipo ya Kielektroniki kutoka TASAF, Josephine Joseph akizungumza kwenye Mkutano wa Misa Tanzania na wadau (MISA-TAN - Wadau Summit 2025) leo Machi 14, 2025, jijini Dodoma
Mratibu wa Malipo ya Kielektroniki kutoka TASAF, Josephine Joseph akizungumza kwenye Mkutano wa Misa Tanzania na wadau (MISA-TAN - Wadau Summit 2025) leo Machi 14, 2025, jijini Dodoma

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kupitia ruzuku wanayotoa kwa kaya masikini, umefanikiwa kuboresha maisha ya kaya maskini nchini kwa kupitia uhawilishaji wa fedha hali ambayo imewezesha asilimia sita ya watoto kuhudhuria kliniki na shuleni ikiwa ni pamoja na kujiunga na vyuo vikuu.

Akizungumza kwenye Mkutano wa Misa Tanzania na wadau (MISA-TAN - Wadau Summit 2025) leo Machi 14, 2025, jijini Dodoma, Mratibu wa Malipo ya Kielektroniki kutoka TASAF, Josephine Joseph amesema TASAF ilianza mwanzoni mwa 2000 ambapo ilijikita kwenye ujenzi wa miundombinu ya shule, elimu na barabara, ila kuanzia 2013 wamejikita katika kuwainua wananchi kiuchumi kwa kuwapatia ruzuku.

Mratibu huyo amesema uamuzi wa kutoa ruzuku umekuwa na matokeo chanya kwa wanufaika wa TASAF hasa katika eneo la afya, elimu na kiuchumi.

"Ruzuku ambayo tunatoa kwa wanufaika wa TASAF imekuwa na matokeo chanya kwenye elimu, afya na kiuchumi, hivyo kutoa tafsiri sahihi ya maendeleo ya Taifa," amesema.

Josephine amesema kupitia TASAF zaidi ya vikundi 68,000 vimeanzishwa nchini kote na kuwa na akiba ya Sh.bilioni 7.8 ambazo zinazunguka kwenye uchumi wa nchi.

Amesema pia wameanzisha afua ya ajira kwa jamii inayonufaika na TASAF, hali ambayo itaongeza mchango kwenye uchumi wa nchi na jamii kwa ujumla.

Aidha, amesema pia TASAF imewezesha watoto wanaotoka familia maskini kupata mkopo kwa asilimia 100 jambo ambalo halikuwepo awali.

Mratibu huyo amesema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2017 hadi 2018 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), ulionesha bila uwepo wa TASAF umaskini ungeongezeka kwa asilimia 7 hadi 8.

"Pia tumeweza kuchochea kaya kuongezeka mapato na matumizi, hali ambayo itachochea ukuaji wa uchumi," amesema.

Akichangia hoja katika mkutano huo, Mhariri Mkuu wa Nipashe Digital, Salome Kitomari amesema TASAF imeweka utaratibu nzuri wa kuifikia jamii kwa kushirikiana na vyombo vya habari.

"Tunaona mnyororo wa thamani kwa wanufaika wa TASAF kwamba si kupewa fedha tu bali kuwawezesha kubadilisha maisha yao na sasa wapo watoto wa maskini wamefikia ndoto zao za kusoma hadi vyuo vikuu,"amesema.

Aidha, amesema mchango wa vyombo vya habari kwenye maendeleo ya kiuchumi ni mkubwa na ndio maana vimekuwa mstari wa mbele kuibua masuala ya kijamii.

Mwenyekiti wa MISA- TAN, Edwin Soko, amesema matarajio yake Kongamano hilo liwepo kila mwaka kwa kujumuisha wadau na wanahabari ili kujadili masuala ya uchumi, siasa na kijamii kwa maslahi ya Taifa.

Soko amesema MISA TAN inatamani kuona kila mdau anaguswa na maendeleo ya nchi, kwa kuelewa msingi sahihi wa kushirikiana.

"Sisi MISA- TAN tunaamini kwenye malumbano ya tija yenye hoja za kujenga Taifa hivyo tunawaomba wadau  kutambua MISA Wadau Summit kama jukwaa la majadiliano ya kimaendeleo na kuleta suluhisho," amesema.

Amesema ushuhuda ulitolewa na TASAF katika kubadilisha maisha ya Watanzania unapaswa kujulikana kwa kila mtu na kupitia kongamano kama hili wananchi watajua.

Picha : MATUKIO YANAYOENDELEA MKUTANO 'MISA - WADAU SUMMIT 2025'

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com