Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo CCM Mkoa wa Ruvuma John Foroteo Haule akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusu ziara ya Katibu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Taifa Dkt Emanuel Nchimbi mkoani Ruvuma

Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo CCM Mkoa wa Ruvuma John Foroteo Haule akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusu ziara ya Katibu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Taifa Dkt. Emanuel Nchimbi mkoani Ruvuma
Na Regina Ndumbaro - Ruvuma
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi ya siku tano mkoani Ruvuma kuanzia Aprili 2, 2025, hadi Aprili 7, 2025.
Ziara hiyo inalenga kuimarisha chama, kuzungumza na wananchi, pamoja na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwa mujibu wa Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa CCM mkoa wa Ruvuma, John Foroteo Haule, Balozi Dkt. Nchimbi ataanza ziara yake kwa kupokelewa Wilayani Tunduru akitokea mkoa wa Mtwara.
Katika kipindi cha ziara yake, atatembelea Wilaya za Tunduru, Namtumbo, Mbinga, Nyasa na Songea Mjini, ambapo atafanya mikutano ya hadhara kwa lengo la kuzungumza na wananchi kuhusu utekelezaji wa Ilani ya CCM na kusikiliza changamoto zinazowakabili.
Mbali na mikutano hiyo, Katibu Mkuu wa CCM pia atakagua na kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo sekta za afya, elimu, barabara, kilimo na maji.
Ziara hii inatarajiwa kutoa fursa ya tathmini ya utekelezaji wa miradi hiyo na kuimarisha ushirikiano kati ya chama, serikali na wananchi katika kuwaletea maendeleo endelevu.
Ziara ya Balozi Dkt. Nchimbi mkoani Ruvuma inatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo na mshikamano ndani ya chama, huku ikitoa mwanga kwa wananchi kuhusu juhudi zinazofanywa na serikali katika kuboresha maisha yao.
Aidha, wananchi wa mkoa huo wanatarajiwa kushiriki kwa wingi katika mikutano ya hadhara ili kupata nafasi ya kuwasilisha maoni yao na kushiriki katika mchakato wa maendeleo ya taifa.
Social Plugin