Habari Mpya

    Loading......

TASAF KUBORESHA ZAIDI AJIRA ZA MUDA MFUPI


Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Shadrack Mziray amesema ziara ya mafunzo nchini, Afrika Kusini kuhusu utekelezaji wa ajira za muda mfupi itawasaidia kuimarisha utendaji.

Viongozi na TASAF  kutoka Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), akiwemo Waziri wa Wizara hiyo George Simbachawene wapo nchini Afrika Kusini kwa mualiko wa serikali hiyo, kupitia Shirika la Kazi Duniani (ILO), ambapo wanajengewa uwezo kuhusu mchakato wa ajira za muda mfupi.

“Kwetu sisi ziara hii, itatusaidia kwa sababu hivi sasa tunakwenda kukamilisha awamu ya pili ya mpango wa kunusuru kaya maskini hapo Septemba,”amesema Mziray katika ziara hiyo iliyoanza Machi 17 hadi 23.

Nakuongeza kuwa, “Lakini tupo katika utaratibu mzima wa kutengeneza programu mpya, hivyo yale tutakayojifunza hapa tutayachukua ili kuboresha kwenye programu mpya ya TASAF inayokuja” .

Amesema Serikali ya Afrika Kusini imewahamasisha kwa namna inavyotekeleza na kutengeneza mradi huo unaotoa fursa nyingi za ajira na ujuzi hasa kwa vijana wanaomaliza vyuo, lakini wanapata changamoto ya kupata ajira.

Mziray amefafanua kuwa vijana pia wanakuwa wamesoma nadharia, sasa wanapata nafasi ya kushiriki kwa vitendo kupitia shughuli mbalimbali zinazotekelezwa.

Kwa upande wake, Waziri Simbachawene amesema wameshiriki mkutano unaohusu ajira zisizo rasmi ambazo Serikali ya Afrika Kusini wameziwekea utaratibu mzuri tangu miaka 20 iliyopita.

Simbachawene amesema kwa sababu ajira hizo, zimeongezewa wigo na hadi kufikia kuwajengea vijana ujuzi, ujasiriamali na kuziba pengo la ukosefu wa ajira.

Katika mafunzo hayo, Simbachawene amesema mbali na kumaliza masomo yao, wahitimu wakiwemo na vyeti vyao, wanashiriki ajira katika kampuni za umma.

“Wenzetu (Afrika Kusini) wana hii programu ambayo inawasaidia sana vijana waliomaliza vyuo, ni kama vile tu Tanzania tulivyotengeneza mtaala ambao tunataka kuutekeleza sasa,”amesema   Simbachawene.

Meneja wa Masijala ya Kumbukumbu za Walengwa Tasaf, Philipine Mmari wa TASAF, amesema taasisi hiyo ilianzishwa mwaka 2000 ikiwa ni njia mojawapo ya kupunguza umasikini na imekuwa na utekelezaji kwa awamu tofauti.

Kwa mujibu wa Mmari, TASAF awamu ya tatu imekuwa na vipengele viwili kikiwemo cha kunusuru kaya za walengwa kilichokwisha mwaka 2019, na sehemu ya pili ilianza mwaka 2019 hadi Septemba 2025.
 
“Katika utekelezaji mpango huu, afua tatu muhimu ikiwemo uahulishaji wa fedha kwa kaya zenye uhitaji, na zile zenye watu wenye ulemavu, afua nyingine ni ajira za muda kwa kaya zenye watu kuanzia umri wa miaka 18 hadi 65,”amesema.

Mmari amesema afua ya mwisho ni kuunda vikundi visivyopungua watu 15 na kuweka akiba kwa ajili kukopeshana.   

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com