



Na Regina Ndumbaro Songea.
Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma kimepongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa juhudi zake katika kuboresha maslahi ya walimu, ikiwemo kupandisha madaraja kwa wakati, kulipa viwango vipya vya mishahara, na kuhakikisha walimu wanapata daraja la mserereko.
Katibu wa CWT Manispaa ya Songea, Neema Lwila, ametoa pongezi hizo wakati wa Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika katika ukumbi wa Anglikana mjini Songea.
Amesema hatua hizo zimeleta faraja kwa walimu na kuimarisha hali yao ya kazi.
Lwila ameeleza kuwa awali walimu waliokuwa na ajira ya pamoja walikuwa wakiachana kimadaraja bila sababu za msingi, lakini sasa hali hiyo imerekebishwa baada ya mazungumzo kati ya Serikali na Chama cha Walimu kupitia Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora.
Amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha shule mpya zaidi ya 600 za msingi na sekondari, kuboresha miundombinu kwa kukarabati madarasa na nyumba za walimu, pamoja na kuajiri walimu wapya.
Pia, amesisitiza kuwa Serikali imeanza kulipa madeni ya walimu, ingawa bado yanadaiwa kwa kiwango kikubwa.
Akizungumzia changamoto za walimu, Lwila amesema Manispaa ya Songea inakabiliwa na uhaba mkubwa wa walimu, ambapo baadhi ya shule zina walimu wasiozidi watano, hali inayosababisha madarasa mengine kubaki bila mwalimu wanapokuwa kwenye vipindi.
Amesema changamoto hii inaathiri ufaulu wa wanafunzi, hasa kwa elimu ya awali na msingi.
Ametoa wito kwa Serikali kuongeza ajira za walimu ili kuboresha kiwango cha elimu.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Msingi wa Manispaa ya Songea, Hossen Mghema, amewataka walimu kuwa wazalendo na kuendelea kuiunga mkono Serikali kwa kuwa imefanya maboresho makubwa kwa walimu katika kipindi cha miaka minne.
Amebainisha kuwa maboresho hayo yamehusisha ujenzi wa nyumba za walimu, kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, pamoja na upatikanaji wa vifaa vya kufundishia.
Amewataka walimu na wanafunzi kutunza miundombinu ya shule zao ili ziweze kudumu kwa muda mrefu.
Mwenyekiti wa CWT Manispaa ya Songea, Emmanuel Komba, ambaye amechaguliwa tena kwa kipindi cha miaka mitano, aliwataka walimu kufanya kazi kwa bidii, uadilifu, na weledi ili kuboresha kiwango cha taaluma na kuepuka migogoro isiyo na tija.
Amewashukuru wanachama wa chama hicho kwa kumuamini na kumuunga mkono kwa mara nyingine, huku akiahidi kutoa ushirikiano mkubwa katika kutetea maslahi ya walimu na kuboresha sekta ya elimu kwa ujumla.
Social Plugin