
Na Lydia Lugakila - Bukoba
Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Mkazi Bukoba mkoani Kagera imeanza kusikiliza kesi nambari 7235 ya uhujumu uchumi inayohusisha washitakiwa wanne wa makosa mbalimbali ya kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Kagera.
Akisoma makosa hayo ,mbele ya hakimu mfawidhi mkazi wa mahakama ya Bukoba Janeth Masesa wakili wa Serikali Judith Mwakyosa amesema washitakiwa hao wamekutwa na makosa tisa ambayo waliyafanya tarehe tofauti huko Wilayani Karagwe.
Amesema,makosa hayo ni kukutwa na bidhaa ambazo hazijasajiliwa,kutengeneza bidhaa ambazo hazina leseni,kushidwa kuwasilisha maombi au tamko,kushindwa kuwasilisha mrejesho wa bidhaa,kushindwa kutunza kumbukumbu,kushindwa kubandika stampu,kushindwa kulipa kodi zaidi ya milioni 10,kusaidia kuwepa Kodi,na Kusababisha hasara Serikalini.
Wakili Mwakyosa amesema,katika kesi hiyo washitakiwa ni Mwesiga Rupia,Nelius Kaizirege, Julieth Ishengoma, Erieth Gerevaz walitenda makosa kwa kujihusisha na ukiukaji wa taratibu na kanuni za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)juu ya ukwepaji wa kodi.
Amesema, washitakiwa wa kwanza na wa pili Mwesiga Rupia na Nelius Kaizirege wanahusika na kosa namba sita ambalo ni kushindwa kubandika stampu za kieletroniki na kosa la saba ambalo ni kushindwa kulipa Kodi na kosa la nane linamhusisha mshitakiwa wa pili kumsaidia Mwesiga Rupia kukwepa Kodi.
Ameongeza kuwa mshitakiwa wa tatu na wanne ambaye ni Julieth Ishengoma na Erieth Gerevaz wamehusishwa na makosa ya kutunza bidhaa ambazo hazina stampu ikiwa maelezo ya kosa ni kwamba nyumbani kwa Juliethi zilikutwa chupa za pombe aina ya jagwa ambazo hazikuwa na stampu.
Hakimu mfawidhi mkazi wa mahakama ya Bukoba Janeth Masesa amesema, mahakama imatoa masharti ya dhamana kwa washitakiwa wanne ikiwa wa kwanza na pili wanatakiwa kuwa na wadhamini wawili wakiwa na sh.milioni 2.6 pamoja na barua na vitambulisho vya makazi endapo watashindwa kufanya hayo walete hati ya kitu kisichohamishika.
Amesema kwa washitakiwa wa tatu na nne kutakuwa kuleta vitambulisho na wadhamini wawili na wao kuhakikisha washitakiwa hao wanafika mahakamani kila wanapohitajika,washitakiwa hao wamepewa dhamana na kesi hiyo itatajwa tena April 8 mwaka huu
Social Plugin