Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BUTONDO ATUA IDUKILO..MAMA LISHE WAMPONGEZA UHAMASISHAJI NISHATI SAFI YA KUPIKIA


Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Kishapu Mkoani Shinyanga Godfrey Mbussa Kwa niaba ya Mbunge wa jimbo hilo Mhe. Boniphace Butondo Machi 25,2025 akikabidhi majiko ya gesi kwa mamalishe wa Kata ya Idukilo kuunga mkono sera ya serikali ya awamu ya sita ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kutunza mazingira kwa kuondokana na ukataji miti hovyo kujipatia kuni na mkaa.
Picha ya pamoja ya Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Kishapu Mkoani Shinyanga Godfrey Mbussa na baadhi ya wajasiriamali Machi 25,2025 wakati ofisi ya Mbunge ikikabidhi majiko ya gesi kwa lengo la kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya sita matumizi ya nishati safi ya kupikia katika Kata ya Idukilo Wilayani Kishapu Mkoani humo.

Na Sumai Salum - Kishapu

Mbunge wa Jimbo la Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe. Boniphace Butondo ametoa majiko ya gesi kwa baadhi ya mama lishe wa Kata ya idukilo Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga.

Akizungumza wakati wa kukabidhi majiko hayo Machi 25,2025 kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo hilo Katibu wa Mbunge Godfrey Mbussa amesema jitihada za Mbunge ni kuhakikisha wananchi wanaijua vizuri na kuiunga mkono sera ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kulinda mazingira.

"Ndugu zangu, Mhe. Butondo ametuma salamu nyingi kwenu na amesema anathamini jitihada zenu za kufanya biashara ili mjipatie kipato kwa maendeleo,leo anawapa majiko haya kwa lengo la nyie kuwa mabalozi wazuri wa nishati safi ya kupikia katika familia na jamii inayowazunguka hivyo mnao wajibu wa kuunga mkono sera hii ili tulinde mazingira yetu",amesema.

Aidha mamalishe hao wamempongeza Mbunge kwa kuwakumbuka na wao wanaishi mazingira ya kijijini ambapo mwanzo walizoea kutumia nishati chafu ya kuni na mkaa kupikia na sasa wanatumia gesi kwani itarahisisha mapishi na kuokoa muda na wataendelea kutoa elimu.

Ni zaidi ya majiko ya gesi 290 aliyogawa Mbunge wa Kishapu kwa wafanyabiashara wa vyakula mijini na vijijini lengo ni kuhakikisha jamii inatumia nishati safi ya kupikia ili kupunguza ama kuondoa uharibifu wa mazingira wa kukata miti kwa ajili ya matumizi ya kupikia ya kuni na mkaa ambayo ni adui wa mazingira na kusababisha ukame na adui wa afya za watumiaji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com