Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

IRELAND YARIDHISHWA NA MRADI WA MAFUNZO KWA WAHUDUMU WA AFYA NGAZI YA JAMII TANGA

Na Hadija Bagasha -  Tanga

WAZIRI wa mambo ya nje ya nchi wa Ireland Neale Richmond, amesema nchi hiyo imeridhishwa na mradi wa mafunzo kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii na itaendelea  kufadhili mpango huo  kusaidia kukabiliana na magonjwa na kuokoa vifo vya wajawazito na watoto.

Ziara ya waziri wa mambo ya nje ya nchi nchini Ireland imefanywa jijini Tanga lengo likiwa ni kuona maendeleo ya mradi wa huduma ya afya ngazi ya jamii ,mradi unaolenga kukabiliana na magonjwa mbalimbali.

Akizungumza mara baada ya kufika katika kituo cha afya cha Mikanjuni Waziri huyo amesema kwamba ni wasaa mzuri sana kusikia kutoka kwa wahudumu wanaofanya kazi ya kutoa huduma  za afya ngazi ya jamii na wale wanaofanya kazi kwenye vituo vya kutolea huduma lakini pia na wale ambao wanasaidia kufanya maisha ya jami kuwa mazuri katika Mkoa wa Tanga.

“Jambo hilo ni muhimu sana  na tuna furaha  ya kuendelea kufadhili mradi huu  na tutaendeklea kushirikiana na serikali ya Tanzania  na taasisi nyingine  kuona  ufadhili unakuwa endelevu,”alisema Waziri huyo.

Kwa upande wa taasisi ya Benjamini Mkapa Foundation wadau kwenye mradi huo, wamesema kupitia mradi wa  afya ngazi ya jamii, jamii inanufaika kiafya, huku watoa huduma wakijivunia mchango wao kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo kuwarudisha kiliniki watoto ambao waliachishwa huduma hiyo kabla ya wakati wao.

Dkt. Helen Senkoro ni Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Benjamini Mkapa Foundation amesema kwamba programu hiyo wanayoitekeleza kwa jamii ni ya Kitaifa na nchi ya Ireland imeahidi kuendelea kusapoti mikakati ya kitaifa kwa kushirikiana na Serikali  pamoja na wadau wengine ikiwemo taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation.

Aidha Dkt Senkoro amesema kwamba sehemu ambazo wamekuwa wakiwawezesha ni kujenga mifumo endelevu ya kutoa huduma za afya ikiwemo upatikanaji wa watumishi ambapo kwa kushirikiana na taasisi hiyo wameweza kuajiri watumishi 450 sehemu mbalimbali nchini ikiwemo bara na visiwani.

“Ireland ni mmoja ya mdau wetu mkubwa ambaye amekuwa anatuwezesha kama taasisi na sisi Mkapa Foundation tumekuwa nao tukishirikiana nao kwa zaidi ya miaka 10 sasa na fedha ambazo wametoa ni takribani bilioni 21 kwa miaka 10 katika kuimarisha huduma za afya,”alibainisha Dkt.Senkoro.

Naye John Sagaika Mratibu wa elimu ya afya ya elimu kwa umma ngazi ya Mkoa amesema wao kama sekta ya afya Mkoa Tanga  wanatoa shukrani kwa ubalozi wa Ireland kwa kufanikisha kupeleka mafunzo kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii 440 ambao wamepata mafunzo kwa miezi 6 miezi mitatu darasani na miezi mitatu kwa vitendo jambo ambalo limekwenda kuleta mtazamo chanya kwa jamii ikiwemo kiubua wagonjwa wapya ngazi ya jamii.

Kwa upande wake Muhudumu wa afya ngazi ya jamii Najma Twalibu amesema kwamba mradi huo umeweza kuwasaidia kwa kiwango kikubwa ikiwemo kupunguza idadi kubwa ya watu wanaoishi kwa matumaini waliopoteza muelekeo kwenye vituo vya afya ambapo kwa huduma zao wanazotoa za nyumba kwa nyumba wameweza kuwapata na kuwarudisha katika vituo vyao na kuendelea kupata huduma.

“Nafurahia sana kuifanya shughuli hii kwakuwa ni shughuli ya kijamii naweza kutoka na kuingia nyumba kwa nyumba na kugundua mahitaji tofauti ya watu wenye rika zote na kuweza kutoa vifaa na kuwafikisha vituo husika kupata huduma stahiki zote kama mtanzania mwenye haki zake za msingi,”alisema Najma.

Ziara hiyo ni sehemu ya ziara ya waziri wa mambo ya nje  ya nchi, nchini Ireland ya kutembelea miji  tisini  duniani ambayo ina miradi  ya afya inayotekelezwa kwa ufadhili wa nchi hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com