Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TRA KAGERA YAENDELEA KUTOA TAHADHARI KWA WANUNUZI WA BIDHAA NA WAUZAJI WANAOKIUKA KUTOA NA KUDAI RISITI ZA KIELEKTRONIKI

 

Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)Mkoa wa Kagera Castro Angelo John akizungumza na Waandishi wa habari

Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)Mkoa wa Kagera Castro Angelo John akizungumza na Waandishi wa habari

Na Lydia Lugakila - Bukoba

Wafanyabiashara Mkoani Kagera  wanaoshindwa kutoa risiti kwa wanunuzi au kutoa risiti isiyo sahihi wamo hatarini kukumbana na faini kubwa kati ya shilingi milioni mbili au kifungo kisichozidi miaka mitatu au adhabu zote mbili.

Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) Mkoa wa Kagera Castro Angelo John wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Akizungumzia masuala mbali mbali yahusuyo umuhimu wa kodi amesema kuwa pia kwa mnunuzi asiyedai risiti atalipa faini ya kiasi kikubwa kati ya 20% ya kodi iliyokwepwa au shilingi elfu 40,000 .

Ameongeza kuwa  umuhimu wa kulipa  kodi ni kuiwezesha Serikali kutoa huduma bora kwa Wananchi.

"Ucheleweshaji wa malipo ya kodi unaambatana na adhabu pamoja na riba iliyowekwa kwa mujibu wa sheria, ambapo riba hutozwa kwa viwango vilivyoidhinishwa na Benki kuu ya Tanzania kwa wakati husika" amesema kiongozi huyo.

Castro ameongeza kuwa kwa mtu atakayeshindwa kuwasilisha ritani kwa wakati atapata adhabu kila mwezi au sehemu ya mwezi atakaochelewa ambapo kwa mtu binafsi kiasi kikubwa kati ya 2.5% ya kiasi cha kodi au shilingi 100,000.00. na kwa kampuni kiasi kikubwa ni kati ya 2.5% ya kiasi cha kodi au shilingi 300,000.00.

Aidha ametoa wito kwa walipa kodi na Wananchi kwa ujumla  kuzingatia muda wa kuwasilisha ritani na kufanya makadirio ya kodi, wenye malimbikizo ya kodi pia watimize wajibu wao kwa kutembelea Ofisi za TRA kujadiliana na kuingia makubaliano ya ulipaji wa kodi bila kuathiri shughuli zao za kiuchumi, 

Amewakumbusha walipa kodi kulipa kodi ya awamu kwa wakati, kutoa risiti ya kielekroniki kila mfanyabiashara anapouza bidhaa au huduma mbali mbali

Vile vile amewakumbusha wanunuzi wote kudai risiti za kielekroniki kwa kila manunuzi ya bidhaa au huduma wanayofanya

Aidha amewashukuru walipa kodi kutoka Wilaya zote za mkoani wa Kagera ambao wamekuwa wakishirikiana na kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi na wajibu mbali mbali kwa mujibu wa sheria  ikiwemo kuleta ritani.

Pia amewashukuru wadau mbali mbali kutoka Ofisi za Serikali hasa mkuu wa Mkoa wa Kagera Hajjat Fatma Mwassa na vyombo vyake pamoja na taasisi mbali mbali za Serikali, taasisi binafsi kwa ushirikiano mzuri.

Pamoja na  hayo amevishukuru vyombo vya habari ambavyo vimekuwa kiungo muhimu katika kuhakikisha walipa kodi wanapata taarifa sahihi pale inapohitajika.
 
"Kodi ni maendeleo ya Nchi tukikusanya kodi tunachochea maendeleo  hivyo kazi hiyo inahitaji mshikamano mkubwa"amesema meneja huyo.

Amesema kuwa huu ni mwezi wa tatu na ni mwezi wa mwisho kwa ajili ya makadilio ya walipa kodi kwa wale ambao mwaka wao wa fedha unaanza mwezi Januari  hadi Desemba.

"kila mwanzoni mwa mwaka mwezi wa kwanza hadi wa tatu walipa kodi wanawajibika kuja kwa ajili ya makadirio, kufanya tathmini ya kodi yao kwa mwaka husika kwa ajili ya kuanza kulipa" amesema Castro.

Amesema kwa kodi ya mapato yatokanayo na biashara, wafanyabiashara binafsi na wadogo wana wajibu wa kufika TRA kufanya makadirio ya kodi miezi mitatu ya mwanzo wa mwaka huku wenye mauzo ya mwaka si zaidi ya shilingi milioni 100 wafike katika ofisi hizo kwa ajili ya kufanya makadirio si zaidi ya Machi 31,2025.

Amewasihi wale wanaoanza biashara kuhakikisha wanafika ofisi za mamlaka hiyo mara tu wanapoanza biashara ili kupata TIN na hatimaye kufanya makadirio ya kodi ya mwaka husika.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com