Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS DKT. SAMIA ATOA ZAWADI YA EID AL FITR KWA WATOTO NA WAZEE - SHINYANGA


Na. Paul Kasembo, SHY RS.

MHE. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa zawadi mbalimbali kwa Makao ya Watoto Yatima (Shinyanga Society For Orphans) iliyopo Bushushu na Makazi ya Wazee na  Wenye Mahitaji Maalum Kolandoto iliyopo Kata ya Kolandoto zote zikiwa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.

Akizungumza baada ya kukabidhi Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amesema kuwa ikiwa ni kuelekea katika Sikukuu ya Eid Al - Fitr, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatambua, anathamini na kuheshimu uwepo wa wao na kwamba yeye mwenyewe na Serikali yake anawapenda na kuwajali wakati wote ndiyo sababu ya kuwapelekea zawadi hizo kwani wao pia ni jamii kama ilivyo jamii nyingine na wanazo haki sawasawa kama binadamu wengine.

"Tunapoelekea katika kuhitimisha Mfungo Mtukufu wa Mwezi wa Ramadhan, nimeelekezwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania niwaletee zawadi zake alizotoa maalum kwa ajili yenu ili katika kusherehekea Sikukuu hii ya Eid Al - Fitr muweze kufurahi pamoja naye kupitia zawadi hizi," alisema RC Macha.

"Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatambua, anathamini na kuheshimu uwepo wenu na kwamba Serikali anayoiongoza itaendelea kuwa karibu na kuishi nanyi wakati wote, aidha itaendelea kusaidizana nanyi katika nyanja na nyakati mbalimbali kutegemea na mahitaji ya wakati husika pia," alisisitiza RC Macha.

Kwa nyakati tofauti Mkurugenzi wa Makao ya Watoto Bibi Haiyamu Said na Msimamizi wa Makazi ya Wazee na Wenye  Mahitaji Maalum Bi. Sophia Kang'ombe wamemshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwathamini, kuwajali na hata kuwapatia zawadi mbalimbali nyakati zote kupitia wasaidizi wake (Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga) na kwamba wao wanamuombea kwa Mwenyezi Mungu awe na afya njema wakati wote ili andelee kuwahudumia wao na Watanzania wote.

Huu ni muendelezo na utaratibu wake Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kutoa zawadi na mahitaji mbalimbali kwa makundi mbalimbali ambapo kwa leo Makao ya Watoto Yatima (Shinyanga Society For Orphans) chenye jumla ya watoto 23 huku Makazi ya Wazee na Wenye Mahitaji Maalum Kolandoto kina wazee 18.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com