
Waziri wa Katiba na Sheria na Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Mkoani Ruvuma Mheshimiwa Damas Ndumbaro Akizungumza leo katika ukumbi wa Manispaa Songea

Na Regina Ndumbaro, Ruvuma
Waziri wa Katiba na Sheria, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini, Mheshimiwa Damas Ndumbaro, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuimarisha haki za wananchi kupitia kampeni ya Mama Samia Legal Aid.
Akizungumza katika Ukumbi wa Manispaa ya Songea, Waziri Ndumbaro amesema kuwa kampeni hiyo imefanikiwa kwa kiwango kikubwa, ambapo hadi sasa imefikia mikoa 22 nchini.
Ameeleza kuwa Samia Legal Aid inalenga kuboresha maisha ya wananchi kwa kuwapatia elimu ya kisheria na kusaidia kutatua migogoro ya ardhi, mirathi, ndoa, na masuala mengine ya kisheria yanayowakabili wananchi wa kawaida.
Waziri Ndumbaro ameongeza kuwa kupitia juhudi za serikali chini ya uongozi wa Rais Samia, sekta ya sheria imeimarika zaidi, huku wananchi wakihamasika kushiriki kikamilifu katika masuala ya kisheria.
Ameeleza kuwa mpango huo wa msaada wa kisheria umeleta mwamko mkubwa kwa wananchi kuelewa haki zao na namna ya kuzidai kupitia vyombo husika.
Aidha, Waziri huyo amesema kuwa utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) umeimarika zaidi katika Mkoa wa Ruvuma, hususan katika Jimbo la Songea Mjini.
Ameeleza kuwa serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya mahakama ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za haki kwa ukaribu zaidi.
Katika hatua nyingine, Waziri Ndumbaro amesema kuwa ujenzi wa Mahakama katika Kata ya Msamala unaendelea vizuri, ambapo jengo hilo litakuwa na ngazi zote za mahakama.
Ameeleza kuwa mradi huo ni moja ya juhudi za serikali za kusogeza huduma za mahakama kwa wananchi, kupunguza msongamano wa kesi, na kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati.
Social Plugin