



***
Na Regina Ndumbaro-Tunduru.
Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Mkoani Ruvuma kimewataka viongozi wa matawi katika shule mbalimbali kuhakikisha wanatenga muda wa kusikiliza na kutatua kero za walimu ili kuongeza morali ya kufundisha.
Wito huo umetolewa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Taifa wa CWT, Sabina Lipukila, wakati wa Mkutano Mkuu wa uchaguzi wa chama hicho uliofanyika wilayani Tunduru.
Lipukila amesema baadhi ya viongozi wanashindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo, jambo linalowafanya walimu kukata tamaa na kushuka kwa morali ya kazi.
Lipukila amesisitiza kuwa viongozi wa matawi wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kusimamia haki za walimu na kushughulikia changamoto zao badala ya kuwalazimisha kufuata huduma katika ngazi za juu.
Ameeleza kuwa baadhi ya walimu wanalazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma ambazo zinaweza kutatuliwa katika ngazi ya shule.
Ametoa wito kwa viongozi wa CWT kuhakikisha kuwa wanajenga mazingira bora ya kazi kwa walimu ili kuwawezesha kujikita katika ufundishaji.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Simon Chacha, amewataka walimu kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kuinua kiwango cha elimu wilayani humo.
Amesema serikali inatambua mchango wa walimu katika maendeleo ya taifa na itaendelea kuwathamini kwa kuhakikisha wanapata mazingira mazuri ya kufundishia.
Chacha amesisitiza kuwa hakuna taifa lolote lililopiga hatua za maendeleo bila kuwa na walimu bora, hivyo aliwataka walimu kuongeza juhudi ili kuhakikisha wanafunzi wanafaulu kwa viwango vya juu.
Katibu wa CWT Wilaya ya Tunduru, Mtamila Abdul, amebainisha kuwa wilaya hiyo ina jumla ya walimu 1,553, ambapo 1,268 kati yao ni wanachama wa CWT.
Amesema chama kimekuwa mstari wa mbele katika kuwatetea walimu kwa kuwapatia ushauri wa kisheria na kusaidia wanachama wenye kesi mahakamani.
Pia, chama kimeshirikiana na serikali kuhakikisha walimu wenye sifa wanapandishwa vyeo na kurekebishiwa mishahara yao, jambo ambalo limeongeza motisha kwa walimu katika utendaji wao wa kazi.
Mtamila ameongeza kuwa CWT imeendelea kusaidia wanachama wake kwa kutoa misaada ya kifedha kwa walimu wenye matatizo mbalimbali.
Pia, ameipongeza serikali kwa juhudi zake za kuboresha sekta ya elimu, ikiwemo kuajiri walimu wapya na kuwapandisha vyeo walimu waliostahili.
Amewataka walimu kuendelea kushirikiana na chama hicho ili kuimarisha mshikamano na kuhakikisha changamoto zinazowakabili zinashughulikiwa kwa ufanisi.
Social Plugin