Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita, akizungumza na wakulima wa pamba na tumbaku akiwataka kusimamia ubora wa mazao yao kuanzia shambani hadi sokoni ili kumfikia mlaji kwa ubora unaotakiwa.
NA NEEMA NKUMBI- KAHAMA
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita, amewataka wakulima wa pamba na tumbaku kusimamia ubora wa mazao yao kuanzia shambani hadi sokoni ili kumfikia mlaji kwa ubora unaotakiwa.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa 29 wa Mwaka wa KACU, uliofanyika Machi 21, 2025, Dc Mboni amesisitiza umuhimu wa uzalishaji bora wa mazao ili wakulima waweze kurejesha mikopo yao na kuongeza thamani ya mazao.
Ameeleza kuwa serikali inatarajia kuona vyama vya ushirika vikisonga mbele kwa kuimarisha shughuli za kilimo na kuhakikisha wakulima wanapata faida inayowasaidia kuondokana na umaskini.
Mboni ameziasa taasisi za kifedha, kama vile mabenki, kushirikiana na kampuni za bima na wadau wengine ili kuendelea kuelimisha wakulima kuhusu bima ya mazao, Hii itasaidia kuhakikisha kwamba mikopo ya benki haiwezi kupotea na wakulima watanufaika pindi yanapotokea majanga kama ukame.
Katika taarifa ya kilimo cha zao la tumbaku, Mwenyekiti wa KACU, Emanuel Nyambi, amesema kuwa walitarajia kuzalisha zaidi ya kilo milioni 20 za tumbaku, lakini kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, ukame na mvua za mawe, wanatarajia kuzalisha kilo milioni 15, ambazo ni pungufu ya makubaliano ya mkataba.
Emanuel amesema ekari 500 za tumbaku zimeharibika, na majani ya tumbaku yamepungua uzito kutokana na ukame.
Mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini, Kibela Kishimba, ameomba chama cha ushirika kuingiza mazao mengine kama mpunga ili wakulima wa mazao mengine nao waweze kunufaika na ushirika.
Vilevile, amewashauri kufanya tafiti za mbolea zinazotumika kidogo ili kupunguza gharama za uendeshaji na ameahidi kushirikiana na Mwenyekiti wa KACU kuhakikisha utafiti unafanyika.
Mjumbe wa mkutano huo, Zawadi Mashauri, amesema kuwa wadau wa mabenki walienda kufanya tathmini baada ya mvua za mawe kunyesha, na wamesema kuwa watarudisha kilichopotea kwa wakulima.
Awali, Mrajisi wa Vyama vya Ushirika, Kakozi Ibrahim, amesisitiza kuwa vyama vyote vya ushirika vyaweze kufanya kazi kwa mfumo wa kidigitali, kujiendesha kibiashara na kuepuka hasara.
Social Plugin