Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DR. MPANGO AWAFARIJI WAFIWA MSIBA WA HAWASSI



Na Mwandishi wetu,Dodoma

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango na Mwenza wake Mama Mbonimpaye Mpango wameshiriki msiba wa Bi. Damaris Hawassi ambaye ni Mke wa Katibu wa NEC (Uchumi na Fedha) wa Chama Cha Mapinduzi Dkt. Frank Hawassi katika makazi ya familia hiyo mtaa wa Miyuji Jijini Dodoma.

Akiwafariji waombolezaji katika msiba huo, Makamu wa Rais ametoa salamu za rambirambi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ametoa salamu za pole kwa familia na waombolezaji wote kufuatia msiba huo.

Makamu wa Rais amewaombea faraja wanafamilia pamoja na wote walioguswa na msiba huo. Amewashukuru wananchi waliojitokeza kuifariji familia katika kipindi hiki kigumu kwao.

Makamu wa Rais amesema ni vema Watanzania kuendelea kushirikiana katika changamoto mbalimbali zinapotokea katika jamii ikiwemo magonjwa na vifo kwa kudumisha undugu, amani na kupendana ili kuwa na Taifa zuri na lenye ustawi.

Halikadhalika Makamu wa Rais amesema Bi.Damaris Hawassi alikua mchapakazi hodari aliyetimiza vema wajibu wake katika umri aliyojaaliwa duniani. Ameongeza kwamba ni vema kujifunza juu ya kila mmoja kutimiza wajibu wake pamoja na kuishi vema na wanadamu wengine.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com