FAMILIA YA MZEE KING MAJUTO YATOA MSAADA WA CHAKULA KITUO CHA WATOTO YATIMA TANGA

Na Hadija Bagasha Tanga, 

FAMILIA ya Marehemu Mzee King Majuto leo wametoa msaada wa vyakula pamoja na vinywaji katika kituo cha kulea Watoto Yatima cha Goodwill Foundation kilichopo Mkoani Tanga ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali kuisaidia Jamii.

Hatua ya msaada huo ni sehemu ya familia hiyo kurudisha kwa jamii baada ya kupokea fedha taslimu kutoka kwa Rais Milioni 30 ikiwa ni kutambua mchango wa mzee wao katika Tasnia ya Filamu hapa nchini.

Akizungumza mara baada ya kugawa msaada huo Mke wa Marehemu King Majuto  alisema wamekwenda kukabidhi sadaka kwa watoto yatima wanaolelewa katika kituo hicho ikiwa ni kuwapunguzia makali ya maisha.

“Tumeona kwenye mwezi mtukufu wa ramadhani mara nyingi katika mwezi huo heri nyingi unazozifanya mwenyezi Mungu anazipokea kwa kushirikiana na Familia tumeona tulifanyie hilo kwa pamoja kuwafikia watoto yatima”Alisema

Awali akizungumza Mwenyekiti wa Wasanii wa Filamu Mkoa wa Tanga Mohamed Amri Majuto alisema waliamua kufanya hilo kutokana na kwamba huo ni mwezi mtukufu wa ramadhani na kumuenzi baba yao Mzee Amri Athumani Amri Maarufu King Majuto kwa kutoa sadaka hiyo kwa watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu.

“Hii itakuwa ni furaha kwa mzee alipo na sisi kama familia tunajisikia faraja na mioyo yao imekuwa misafi na haya mambo tumekuwa tukilifanya kila wakati na hata mwezi Agosti kila mwaka tumekuwa tukilifanya kumbumbuka mzee wetu kule kwenye malazo yake”Alisema Mohamed Amri Majuto ambaye pia ni Mtoto wa Mzee Majuto.

Awali akizungumza mtoto mwengine wa Mzee Majuto Othumani Amri alisema lengo kubwa ni kutoa shukrani za dhati Rais Samia Suluhu kuwakabidhi fedha taslimu milioni 30 nao wakaona wafanye suala la kumuenzi mzee kutoa sadaka kwenye kituo cha Watoto Yatima.

“Tunamshukuru Rais Dkt Samia Suluhu kumuenzi mzee wetu pamoja na kutukabidhi kiasi cha Milioni 30 na sisi wakaamua kuenzi mzee wao kwa kutoa sadaka kwenye kituo cha watoto yatima hivyo wanamshukuru kwa kumuenzi mzee wao”Alisema

Awali akizungumza  ni Katibu wa Taasisi ya Nasimama na Mama Popote Alipo  Raphael Kiango alisema wanamshukuru Rais Dkt Samia Suluhu na wameona ni matunda ya moja kwa moja yanayotokana na  Serikali ya awamu ya sita kwa kuthamini mchango wa wasanii ambao hawapo nao kwenye ulimwengu wa sasa.

Alisema lakini wameamua kumpa tunzo ya heshima na kumpatia kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya familia na hivyo kuleta chachu hamasa kwa wasanii jambo ambalo limepelekea familia hiyo kuamua kutoa sadaka.

“ Tunaishukuru Serikali kwa kumpatia tuzo ya heshima Mzee Wetu King Majuto na kutoa kiasi cha Fedha Milioni 30 hivyo kwetu sisi imekuwa ni faraja kubwa kuona namna jina lake linaishi na tunampongeza Rais Dkt Samia Suluhu ,Wizara ya Habari ,Utamaduni Sanaa na Michezo kuwathimini wasanii hata wale ambao wametangulia mbele za haki”,Alisema

Hata hivyo kwa upande wake Mkurugenzi wa Goodwill foundation Sayyed Muhdhar alisema lengo la kuanzishwa taasisi hiyo ni kuisaidia jamiii ikilenga yatima, wazee wasiojiweza na wahitaji huku wakiishukuru familia ya Marehemu Mzee King Majuto kwa kuweza kumfanya mzee majuto kuendelea kuishi.

Alisema kwamba ujio wao umekuwa mzuri kutokana na kuendelea kuenzi aliyokuwa akiyafanya mzee wao kwa kujitolea ikiwemo kuipongeza familia yao kwa kuendelea kumuenzi kumfanya aendelee kuishi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com