
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Bukoba, kupitia Idara ya Sikio, Pua na Koo (ENT), imeadhimisha Siku ya Usikivu Duniani kwa kutoa elimu kuhusu usikivu na huduma za uchunguzi wa masikio bure kwa watumishi wa hospitali hiyo.
Maadhimisho hayo yalilenga kuongeza uelewa juu ya afya ya masikio na kuhamasisha hatua za kujikinga dhidi ya matatizo ya usikivu.
Akitoa elimu ya Usikivu kupitia kitengo cha Habari na Uhusiano BRRH, Daktari Bingwa wa Sikio, Pua na Koo wa hospitali hiyo, Dkt. Richard Shija amebainisha sababu mbalimbali zinazopelekea kupungua kwa usikivu.
"Zipo sababu mbalimbali zinazopelekea tatizo la usikifu hafifu miongoni mwao ni kusikiliza muziki kwa kutumia vifaa vya masikioni (earphones) kwa sauti kubwa, kuchokonoa masikio kwa kutumia vijiti au funguo, kuwepo kwa uchafu mwingi masikioni pamoja na umri mrefu kwani kadri mtu anavyozidi kukua, uwezo wa kusikia upungua na kukaa kwenye maeneo yenye kelele nyingi"
Dkt. Shija alisisitiza madhara ya kutumia vifaa visivyo salama kusafisha masikio nayo upelekea usikivu hafifu huku akieleza kuwa vifaa hivyo vinaweza kuingiza bakteria na fangasi na hatimaye kupelelea kutoboka kwa ngoma ya sikio na matatizo ya usikivu kwa ujumla.
Ameongeza kuwa, Wananchi wanaopata ajali hasa eneo la kichwa kuvunjika kwa mfupa wa sikio na wamekuwa miongoni mwa wanaokumbana na tatizo la usikivu,
Dkt. Shija kupitia siku hii muhimu ametoa rai kwa Wazazi, Walezi na walimu kuepuka kuwapiga watoto makofi kwenye eneo la sikio kwani inaweza kusababisha kupasuka kwa ngoma ya sikio na matatizo ya usikivu.
Naye Muuguzi Kiongozi wa Kitengo cha Sikio, Pua na Koo katika hospitali hiyo, Bi. Theodosia Katebeleza, amewahimiza wananchi kuepuka kuweka maji au mapovu ya sabuni kwenye masikio wakati wa usafi wa mwili huku akisisitiza kuwa makini wanapoenda saluni kunyoa nywele au kusuka kuhakikisha kwamba kemikali zinazotumiwa haziingii masikioni kwani nazo husababisha matatizo ya usikivu.
Siku ya Usikivu Duniani huadhimishwa Machi 3 ya kila mwaka l na kwa mwaka huu, kaulimbiu ni "Badili Mtazamo, Chukua Hatua Binafsi," ikihimiza jamii kuchukua hatua za kujilinda na kuboresha afya ya usikivu.
Social Plugin