Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Serikali imesema ina mpango wa kuboresha Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kuijenga upya ili kuwezesha huduma zote kutolewa ndani ya jengo moja litakalokuwa na vitanda 1,757 kutoka 1,435 vya sasa.
Aidha Upembuzi yakinifu wa mradi huu umekamilika ambapo hatua mbalimbali za kusaini mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Korea zinaendelea ambapo utagharimu USD. 468 Mil. (takriban TZS. 1.2 Tril kati ya hizo USD. 364 Mil zitatoka Korea Kusini na Serikali ya Tanzania itachangia USD. 104 Mil.
Hayo yameelezwa leo March 6,2025 Jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Rachel Mhaville wakati wa akizungumza na waandishi wa habari, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo Prof. Mohamed Janabi, kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Taasisi hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu sita katika Ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, Dodoma.
Dkt. Mhaville amesema utekelezaji wa mradi huo ni wa awamu moja ambao utachukua miaka mitano kukamilika baada ya kusaini mkataba, hautaathiri utoaji huduma.
Amesema Utekelezaji wa mradi huo wa kihistoria katika sekta ya afya nchini utakua na faida lukuki ikiwamo kuboreshwa kwa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi kupitia vifaa tiba vya kisasa ambapo Serikali itapunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya fedha kusafirisha wagonjwa nje ya nchi, kuwezesha wagonjwa kupata huduma zote katika eneo moja, kupunguza mizunguko na usumbufu pamoja na kuwa mpangilio mpya wa hospitali huku eneo kubwa likibaki wazi, kwa matumizi ya maendeleo mengine miaka 50 ijayo
Mkurugenzi huyo wa Huduma za Upasuaji ya Muhimbili amesema Taasisi hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita yenye kampasi mbili, ni Hospitali ya Rufaa ya Kitaifa na kubwa kuliko zote nchini yenye vitanda 2,043 ambapo Upanga kuna vitanda 1,435 na Mloganzila vipo 608.
"Katika Kampasi zote mbili Wagonjwa 4,000 wanaonwa kwa siku ambapo Upanga jumla ya wagonjwa 2,700 wanahudumiwa ikiwa ni wagonjwa wa nje 1,700 na wagonjwa waliolazwa wodini wakati wote ni 1,000,Kampasi ya Mloganzila inahudumia jumla ya wagonjwa 1,300 kwa siku sawa na wagonjwa wa nje 800 hadi 1,000 na wagonjwa 400 waliolazwa, "amesema
Amesema Hospitali ina jumla ya wafanyakazi 3,884 wakijumuisha madaktari, wauguzi, wafamasia, watalaam wa maabara na wafanyakazi wengine. Kampasi ya Upanga ina wafanyakazi 2900 na Mloganzila 984.
Amesema katika maboresho ya huduma Serikali imeongeza vifaa tiba vyenye uwezo mkubwa wa kuchakata sampuli za maabara takribani 2,500 kwa saa moja ili kuongeza upatikanaji haraka wa majibu na kupata matibabu mapema kwa wagonjwa wa nje waliolazwa. Vifaa hivyo vina thamani ya TZS. 1.8 Bilioni.
"Upatikanaji wa vifaa hivi umerahisisha utoaji wa majibu kwa haraka, magonjwa kugundulika haraka, kupunguza muda wa wagonjwa kusubiri matibabu na kuwezesha upatikanaji wa huduma za kibobezi ikiwemo upandikizaji mimba (IVF), upandikizaji figo na uloto" amesema.
Katika jitihada za Serikali za kuthibitisha ubora wa vipimo na majibu yanayotolewa na maabara zetu kwenye viwango vinavyokubalika kimataifa ili kutumika na mamlaka au taasisi yoyote duniani Serikali, imeendelea kuboresha maabara zetu na hatimaye kwa mara nyingine Shirika la Viwango vya Ukaguzi Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADCAS) liliweza kutunuku cheti cha Ithibati ya Ubora wa Maabara (ISO 15189:2022) kwa Kampasi ya Upanga na Mloganzila.
"Ili kuhakikisha ubora wa huduma zinazotolewa, hospitali imeanzisha Benki ya kuhifadhi sampuli na vimelea kwa ajili ya tafiti na kufanikiwa kuanzisha benki ya kuhifadhi sampuli kwa ajili ya mafunzo na tafiti za kisayansi mbalimbali wa vimelea vya magonjwa kupitia maabara kuu ,ikiwa ni ya kwanza katika hospitali za umma iliyolenga kuboresha huduma za tafiti za kisayansi na mafunzo, "amesema.
Kuhusu ununuzi wa Vifaa Tiba vya Uchunguzi, Tiba kupitia Mionzi na Mawimbi amesema Serikali imenunua na kusimika mtambo wa kisasa wa Tiba Radiolojia uliogharimu TZS. 2 Bil.ambao umewezesha hospitali kutoa matibabu ya ubingwa bobezi ambayo yalikuwa hayapatikani hapa nchini na kuongeza idadi ya aina za matibabu ya kibobezi katika eneo hilo ambapo takribani wagonjwa 2,300 wamehudumiwa tangu ulipofungwa mwaka 2022.
"Kupitia mtambo huo, kwa mara ya kwanza nchini, Hospitali imefanikiwa kuanzisha huduma mpya za kuweka mirija myembamba (catheters) kwa kutumia matundu madogo, kutoa damu iliyoganda katika mishipa ya damu na nyinginezo nyingi ambazo zinafanyika kwa ustadi wa hali ya juu," amefafanua
Amesema Serikali ilinunua mashine mpya ya Mammography iliyogharimu TZS 1.8 Bi. ambayo ina uwezo wa kupima na kutoa picha zinazoweza kugundua uvimbe kwenye matiti ukiwa katika hatua za awali kabisa. Aidha jumla ya wagonjwa 810, wamehudumiwa kwa kutumia mashine hiyo tangu iliponunuliwa mwishoni mwa mwaka 2024.
Amefafanua kuwa Mashine hii ambayo ni kisasa na pekee kwa hospitali za umma, inatumiwa na madaktari wabobezi wa radiolojia ya wanawake imeleta mapinduzi ya utoaji wa huduma za uchunguzi wa kisasa kwa wenye magonjwa ya matiti nchini.
Ametaja mafanikio mengine ni kuongeza mashine moja ya CT-Scan (dual) iliyogharimu TZS. 1.8 Bil,kuongeza mashine moja ya MRI yenye nguvu sumaku ya 1.5T ambayo inaweza kuona uvimbe mdogo kabisa katika kupiga picha za uchunguzi iliyogharimu TZS. 2.6 Bilioni na Mashine ya Kidigitali ya X-Ray iliyogharimu kiasi cha TZS. 358 Mil. ambapo kutokana na uwekezaji huo, Hospitali imefanikiwa kupunguza muda wa kutoa majibu ya radiolojia kutoka saa 48 hadi 24 tangu mgonjwa anapopima.
Pamoja na hayo amesema mafanikio mengine ni Uanzishwaji huduma mpya za kibobezi ili kupunguza rufaa nje
ya nchi ikiwemo Uanzishwaji Huduma za Kupandikiza Mimba (IVF)
Septemba 2024.
"Serikali ilifanikiwa kwa mara ya kwanza kuanzisha kituo cha upandikizaji mimba katika hospitali za umma nchini ambacho hadi kukamilika ikiwamo ujenzi, vifaa na kusomesha watalaam vimegharimu TZS. 1.72 Bil,tayari kituo hicho kimeanza kutoa huduma za kuvuna mbegu za kiume na za kike na kupandikiza mimba kwa kina mama wenye changamoto ya kupata watoto kwa njia ya kawaida,"amesema
Dkt. Mhavile amefafanua kuwa Katika kipindi cha miezi mitatu tangu kuanzishwa huduma hiyo, familia zaidi ya nane zimejitokeza kupata huduma hiyo.
Katika kutekeleza azma ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kupambana na magonjwa yasiyoambukiza, hospitali ilifanikiwa kuanzisha matibabu ya kupunguza uzito kwa wananchi wenye uzito uliopitiliza kwa njia ya uwekaji puto katika mfuko wa chakula kutumia endoskopia na wengine kupunguza ukubwa wa tumbo kupitia upasuaji wa matundu madogo.
" Hadi sasa wananchi 155 wamewekewa puto, 44 wamefanyiwa marekebisho ya puto kulingana na uhitaji wa mteja na 11 wametolewa puto, "ameeleza.
Social Plugin