NA NEEMA NKUMBI- KAHAMA
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI imeielekeza Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kumchukulia hatua za kinidhamu Mkandarasi M/S Sichuan Road and Bridge Corporation Ltd, anayetekeleza ujenzi wa barabara na miundombinu mingine ya Manispaa ya Kahama.
Maelekezo haya yametolewa Machi 17, 2025, na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mheshimiwa Justin Nyamoga, wakati wa ziara ya kamati kukagua mradi wa ujenzi wa miundombinu katika Mradi wa TACTIC wilayani Kahama.
Nyamoga amesema kuwa kamati haijaridhishwa na utendaji kazi wa mkandarasi huyo na imeitaka TAMISEMI kuchukua hatua za haraka ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati, kwani Miradi hiyo ikikamilika inatarajiwa kusaidia kukuza uchumi wa Mkoa wa Shinyanga, kuboresha miundombinu, na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi.
Mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini, Kibela Kishimba, ameeleza kuwa mkandarasi huyo amekuwa kero kwa wananchi, akisema kuwa hata wale wanaotoa vifaa kama kokoto, sementi, mafuta na mchanga wanamdai fedha pia ameiomba TAMISEMI kufikiria kubadilisha mkandarasi ili kumaliza changamoto hiyo.
Naibu Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Zainab Katimba, amesisitiza kuwa wasimamizi wa mradi wanawajibika kusimamia miradi kwa ufanisi ili iweze kukamilika kwa wakati na ameongeza kuwa miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia kama TACTIC ina fedha za kutosha, hivyo inapaswa kukamilika kwa wakati ili kunufaisha wananchi.
Mhe. Katimba pia ametoa maelekezo kuwa wakandarasi wanaoshindwa kutekeleza wajibu wao kwa wakati watafungiwa kazi kwa kutozingatia mkataba.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, ameeleza kuwa mkoa huo unaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo kwa fedha kutoka serikali kuu na mapato ya ndani ambapo amefafanua kuwa miradi ya miundombinu ya barabara, ujenzi wa kituo cha mabasi na masoko kwa awamu ya kwanza na ya pili inagharimu shilingi bilioni 48.3.
Mradi huu wa ujenzi wa miundombinu ya barabara ulitarajiwa kukamilika Februari 19, 2025, lakini hadi sasa haujakamilika na Mkandarasi amepatiwa muda wa ziada wa miezi mitatu na anatarajiwa kumaliza mradi na kukabidhi kazi ifikapo Mei 19, 2025.
Social Plugin