Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma Ngolo Malenya kulia,akikata utepe kuzindua rasmi Basi la Chama cha Walimu Wilayani humo ambalo litasaidia kurahisisha utendaji wa majukumu ya chama hicho,kushoto Katibu wa CWT Mkoa wa Ruvuma,wa pili kushoto Mjumbe wa kamati ya Utendaji Taifa anayewakilisha Mkoa wa Ruvuma Sabina Lipukila na Mwenyekiti wa Chama hicho
Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma Ngolo Malenya wa tatu kushoto,akiwa na baadhi ya Viongozi wa Chama cha Walimu Mkoa wa Ruvuma baada ya kufanya uzinduzi wa Basi la Chama cha Walimu Tanzania( CWT )Namtumbo
Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma Ngolo Malenya,akiwasha gari la Chama cha Walimu Tanzania(CWT) ambalo limenunuliwa na Chama hicho ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu kwa Wanachama na Viongozi wa Chama cha Walimu Wilayani humo.
Na Regina Ndumbaro- Namtumbo .
Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Ngolo Malenya, amezindua gari jipya la Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wilayani humo, ambalo litatumika kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya chama na kutoa huduma kwa wanachama wake.
Uzinduzi huo umefanyika katika hafla maalum, ambapo Malenya aliipongeza CWT kwa hatua hiyo muhimu inayolenga kuboresha ustawi wa walimu na jamii kwa ujumla.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Malenya amewataka waajiri katika wilaya hiyo kuhakikisha wanaajiri madereva wenye sifa na wanaozingatia sheria za barabarani ili kuepusha ajali zisizotarajiwa.
Pia amewasihi viongozi wa chama hicho kutunza gari hilo ili liweze kutekeleza majukumu yake kwa muda mrefu bila changamoto.
Katibu wa CWT Wilaya ya Namtumbo, Deograsias Haule, ameeleza kuwa gari hilo limegharimu shilingi milioni 77, ikiwa ni pamoja na gharama za ununuzi, marekebisho, na bima.
Amesema awali chama kilikabiliwa na changamoto ya usafiri, hasa pale wanachama walipohitaji msaada wa dharura, kama vile kuhudhuria misiba.
Hivyo, ununuzi wa gari hilo utapunguza changamoto hizo na kusaidia wanachama kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CWT Taifa anayewakilisha Mkoa wa Ruvuma, Sabina Lipukila, amesema chama hicho kimekuwa mstari wa mbele kutatua changamoto za wanachama wake.
Amesema hadi sasa, wilaya nne kati ya sita za mkoa huo tayari zimenunua mabasi, huku wilaya zilizobaki zikiendelea na mchakato wa ununuzi.
Amesisitiza kuwa mabasi haya ni sehemu ya mkakati wa chama kuhakikisha walimu wanapata usafiri wa uhakika kwa ajili ya shughuli zao za kitaaluma na kijamii.
Lipukila ameeleza kuwa mabasi haya yatasaidia kupunguza gharama za usafiri kwa walimu, hasa wakati wa safari za mafunzo na shughuli nyingine muhimu za chama.
Amesema walimu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kuchangia gharama kubwa za usafiri, lakini kwa hatua hii, chama kitahakikisha wanachama wake wanapata huduma bora na kwa gharama nafuu.
Uzinduzi wa gari hili ni hatua muhimu kwa walimu wa Namtumbo, kwani utarahisisha shughuli za chama na kuboresha mazingira ya kazi kwa wanachama wake.
Viongozi wa CWT wamewataka walimu kuendelea kushirikiana na chama chao ili kuhakikisha wanapata haki zao na kunufaika na miradi inayotekelezwa kwa maendeleo yao.
Social Plugin