Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ODDO MWISHO AENDELEA NA ZIARA YAKE KATIKA WILAYA YA TUNDURU

Mwenyekiti Wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa Oddo Mwisho akizungumza na wananchi wa Kata ya Matemanga iliyopo Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma
Mwenyekiti Wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa Oddo Mwisho akizungumza na wananchi wa Kata ya Matemanga iliyopo Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma
Wananchi waliojitokeza kumsikiliza Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa Oddo Mwisho pichani hayupo katika Kata ya Matemanga Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma
Wananchi waliojitokeza kumsikiliza Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa Oddo Mwisho katika Kata ya Matemanga Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma
Wananchi wa Kata ya Namwinyu walijitokeza kumsikiliza Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa Oddo Mwisho 
 
Na Regina Ndumbaro Tunduru. 

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Ruvuma, Mheshimiwa Oddo Mwisho, ameendelea na ziara yake kwa kuwatembelea wananchi wa Kata ya Namwinyu na Kata ya Matemanga, zilizopo Tarafa ya Matemanga, Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma. 

 Akiwa katika ziara hiyo, amewashukuru wananchi kwa ushirikiano wao mkubwa uliofanikisha ushindi mnono wa CCM katika uchaguzi uliopita. 

Aidha, amesisitiza mshikamano na umoja ndani ya chama ili kuhakikisha maendeleo ya wananchi yanaendelea kuimarika kwa kasi zaidi.

Katika hotuba yake, Mheshimiwa Oddo ametoa tahadhari kuhusu ugonjwa wa Mpox, akiwataka wananchi kuwa waangalifu na kuchukua hatua za kujikinga na ugonjwa huo. 

Amesisitiza umuhimu wa elimu ya afya kwa wananchi na kuwahimiza viongozi wa serikali za mitaa kushirikiana na wananchi katika kuhakikisha afya bora kwa jamii. 

Pia, amewataka wananchi kufuata miongozo ya wataalamu wa afya ili kudhibiti maambukizi ya magonjwa mbalimbali.

Mwenyekiti huyo pia amekemea vikali vitendo vya rushwa ndani ya chama na serikali, akisisitiza kuwa tabia hiyo haikubaliki kwani inakwamisha maendeleo ya wananchi. 

Ameeleza kuwa viongozi wa vijiji wanapaswa kuwa waadilifu kwa kuhakikisha uwazi katika utoaji wa taarifa za mapato na matumizi ya vijiji vyao. 

Amesema wananchi wana haki ya kufahamu maendeleo ya miradi inayotekelezwa katika maeneo yao na kuwa uwazi huo utaimarisha imani ya wananchi kwa serikali na chama.

Aidha, Mheshimiwa Oddo ameeleza kuwa Chama cha Mapinduzi kimeendelea kuwa imara katika kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali. 

Amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, hataki migogoro ndani ya chama, na badala yake anasisitiza mshikamano na maelewano. 

Amesisitiza kuwa changamoto zozote zinazojitokeza zinapaswa kutafutiwa suluhisho ndani ya chama kwa kushirikiana na wananchi.

Katika hitimisho lake, Mwenyekiti Oddo amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa anazozifanya kuwaletea wananchi maendeleo katika sekta mbalimbali kama elimu, afya, umeme na maji. 

Vilevile, amempongeza Waziri wa Afya na Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama, kwa kazi nzuri anayoifanya kuboresha sekta ya afya nchini. 

Amewaomba wananchi kuendelea kushirikiana na serikali na kuunga mkono juhudi za maendeleo, huku akiwahimiza kuendelea kukiamini Chama cha Mapinduzi kwa ustawi wa taifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com