Na. Peter Haule, Rorya Mara, WF
Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya Mkoani Mara wametakiwa kujua kiwango cha juu cha riba kinachopaswa kutolewa kisheria na vikundi na watoa huduma ndogo za fedha ili kutoingia kwenye mikopo yenye riba kubwa itakayosababisha washindwe kurejesha mikopo.
Hayo yameelezwa na Kiongozi wa Timu ya Wataalamu wa Elimu ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro, alipokuwa akitoa elimu ya Fedha kwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya.
Bw. Kimaro alisema kuwa kuna kiwango cha juu cha riba ambacho Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeweka kwa watoa huduma ndogo za fedha ambacho hutolewa kabla ya mtoa huduma kupewa leseni na ndicho kinachostahili kutozwa mtu anapochukua mkopo.
“Ukiachana na mabenki, kiwango cha juu cha riba kinachopaswa kutozwa na watoa huduma ndogo za fedha na vikundi ni asilimia 3.5 kwa mwezi na kwa mwaka ni asilimia 42, kinyume na hapo ni kukiuka miongozo na taratibu za huduma hiyo”, alisema Bw. Kimaro.
Alisema kabla ya kuchukua mkopo ni vema kujilidhisha na kiwango cha riba na pia ukopaji uelekezwe kwenye kuzalisha kitu ambacho kitaweza kurejesha mkopo kwa muda uliowekwa na iwapo mkopo umechukuliwa kwa shughuli za kijamii ni vema kukawa na chanzo kingine cha mapato ambacho kitaweza kurejesha mkopo huo bila kuathiri familia.
Aidha alisema kuwa kabla ya kukopa ni vema kusoma mkataba vizuri na iwapo haujaeleweka mkopaji anatakiwa kupata ushauri kwanza ili kuepuka kuingia kwenye hasara.
Vilevile aliwataka watumishi kufuatilia michango inayotakiwa kuwasilishwa na Mwajili kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, kwa kuwa iwapo kutakuwa na miezi ambayo mchango haujawasilishwa itasababisha usumbufu wakati wa kudai mafao mtumishi anapostaafu.
Kwa upande wa uwekezaji, Afisa Masoko Mwandamizi wa Kampuni ya Uwekezaji wa UTT AMIS, Bw. Rahim Mwanga, alisema kuwa uwekezaji unafanyika ili kutunza thamani ya fedha kwa kuwa fedha ina tabia ya kupungua thamani kadri miaka inavyosogea.
Bw. Mwanga aliwataka watumishi kuwekeza kwenye Hati Fungani za Serikali na Hisa ili kuwa sehemu ya umiliki wa Kampuni ambapo inasaidia kupata faida kupitia gawio na kuuza Hisa wakati inapopanda thamani.
Alisema kuwa kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam kuna Kampuni 28 ambazo mtumishi anaweza kuwekeza ikiwa ni pamoja na kampuni za ndani na nje ya nchi ambapo uwekezaji kwenye Hisa unatakiwa kuwa wa muda mrefu kwa kuwa Hisa zina tabia ya kupanda na kushuka.
Kwa upande wa watumishi wa Wilaya hiyo, waliipongeza Serikali kwa mpango huo wa kutoa elimu ambapo wameeleza kuwa elimu hiyo ingewahi ingewanusuru watumishi wengi hususani wa umma kuingia kwenye migogoro na umasikini kutokana na kukosa elimu sahihi kuhusu mikopo na uwekezaji na pia kujiwekea mazingira mazuri kabla ya kustaafu.
Kiongozi wa Timu ya Wataalamu wa Elimu ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro (kulia), akitoa elimu ya fedha kwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, ambapo amewataka kutambua kiwango cha juu cha riba kinachopaswa kutozwa na vikundi na watoa huduma ndogo za fedha ambacho ni asilimia 3.5 kwa mwezi, elimu hiyo ilitolewa katika Ofisi za Halmashauri hiyo, Mkoani Mara.
Mchumi wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bi. Grory Uiso, akieleza kuhusu taarifa zilizo katika vipeperushi kuhusiana na elimu ya fedha, wakati wa zoezi la kutao elimu kwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Mkoani Mara, lililofanyika katika Ofisi za Halmashauri hiyo, Mkoani Mara.
Afisa Masoko Mwandamizi wa Kampuni ya Uwekezaji wa UTT AMIS, Bw. Rahim Mwanga, akieleza maeneo ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na Hati Fungani za Serikali na Hisa, kwa Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Mkoani Mara.
Timu ya Wataalamu wa Elimu ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, ikiongozwa na Bw. Salim Khalfan Kimaro (wa pili kulia), ikieleza kuhusu program ya utoaji wa elimu ya fedha na lengo lake, wakati wa zoezi la kutoa elimu kwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya Mkoani Mara, lililofanyika katika Ofisi za Halmashauri hiyo.
Afisa Utumishi Mwandamizi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Bi. Caritas Ilahuka (kulia) na watumishi wenzake wakisoma kipeperushi kinachoelezea elimu ya fedha, wakati wa zoezi la kutoa elimu kwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Mkoani Mara, lilofanyika katika Ofisi za Halmashauri hiyo, Mkoani Mara.
(Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha, Rorya)
Social Plugin