Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI KUBORESHA HUDUMA YA MAJI KWA WAKAZI WA MBINGA


Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma Kisare Makori,akizungumza na watumishi wa Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira katika Mji wa Mbinga(Mbiuwasa) na Wakandarasi waliopata kazi ya kutengeneza mabomba na ujenzi wa mradi wa kuboresha huduma ya maji katika mji huo,kulia Mkurugenzi Mtendaji wa Mbiuwasa Mhandisi Yonas Ndomba na kushoto Mwenyekiti wa Bodi ya Mbiuwasa Mhandisi Patrick Ndunguru.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira katika Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma(Mbiuwasa)na Mhandisi Yonas Ndomba kushoto na mwakilishi wa kampuni ya Simba Pipe Industries Ltd Elias Nyenzi,wakionyesha mikataba ambapo kampuni ya Simba Pipe Industries Ltd imepata kazi ya kutengeneza na kusambaza mabomba ya maji kwa ajili ya uboreshaji wa huduma ya maji katika mji wa Mbinga.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbinga mji Mbiuwasa Mhandisi Patrick Ndunguru,akizungumza baada ya Mamlaka hiyo kutiliana saini na wakandarasi.

Na Regina Ndumbaro-Mbinga. 

Serikali imetenga zaidi ya Shilingi bilioni 4 kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji safi na salama kwa wakazi zaidi ya 60,868 wa kata nane katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga, mkoani Ruvuma. 

Mradi huu unahusisha ujenzi wa vyanzo viwili vya maji vyenye uwezo wa kuzalisha lita 1,613,200 kwa siku, matenki manne yenye ujazo wa lita 525,000, pamoja na mtandao wa mabomba wa kilomita 57. 

Lengo ni kuhakikisha huduma ya maji inafikia asilimia 97.8 katika maeneo yanayonufaika na mradi huu.

Katika hafla ya utiaji saini wa mikataba, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mbinga (Mbiuwasa), Mhandisi Yonas Ndomba, ameeleza kuwa mradi huu utapunguza upungufu wa maji uliopo kwa sasa, ambapo mahitaji ni lita 5,478,000 kwa siku lakini uzalishaji ni lita 3,797,000 pekee. 

Kampuni ya Ngogo Engineering Ltd itatekeleza ujenzi wa mradi kwa gharama ya Shilingi milioni 755,194,120.25, huku kampuni ya Simba Pipe Industries Ltd ikihusika na kutengeneza na kusambaza mabomba kwa gharama ya Shilingi bilioni 3,255,414,297.38.

Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Kisare Makori, amezitaka kampuni husika kuhakikisha wanakamilisha mradi kwa wakati na kwa viwango bora. 

Amesisitiza kuwa utekelezaji wa mradi huu utasaidia kufanikisha malengo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, ambayo inalenga kufikisha huduma ya maji kwa asilimia 95 mijini na 85 vijijini ifikapo mwishoni mwa mwaka huu. 

Kupitia mradi huu, Mbinga Mji inatarajiwa kufikia asilimia 98.3 ya upatikanaji wa maji safi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Mbiuwasa, Mhandisi Patrick Ndunguru, amewataka watendaji wa mamlaka hiyo kumsimamia mkandarasi kwa karibu ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na wananchi wanapata maji bila kuchelewa. 

Aidha, amesisitiza umuhimu wa jamii kushiriki katika utunzaji wa vyanzo vya maji na miundombinu ya mradi ili iweze kudumu kwa muda mrefu.

Wakazi wa Mbinga, hususan wa kata ya Masumuni, wameipongeza Serikali kwa hatua hii, wakisema kuwa itasaidia kutatua changamoto ya mgao wa maji uliokuwa ukiwakabili kwa muda mrefu. 

Moses Mapunda, mkazi wa eneo hilo, amesema kuwa kukamilika kwa mradi huu kutakuwa suluhisho la kudumu kwa changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama katika kata zote zinazohusika na mradi huu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com