Mbunge wa Jimbo la Madaba Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kipingo kilichopo katika Halmashauri ya Madaba Mkoani Ruvuma
Wananchi wa kijiji cha Kipingo waliojitokeza kumsikiliza Mbunge wa Jimbo la Madaba Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama
Na Regina Ndumbaro-Madaba.
Kijiji hiki kimekuwa miongoni mwa maeneo yaliyonufaika na miradi mbalimbali ya maendeleo, inayotekelezwa kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mtendaji wa Kijiji cha Kipingo, Ndugu Mohamed Mohamed Ally, akisoma taarifa mbele ya Mbunge wa Jimbo la Madaba, Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama, amesema kuwa miradi iliyotekelezwa katika kijiji hicho kuanzia mwaka wa fedha 2020/21 hadi 2023/24 imejikita katika sekta mbalimbali muhimu.
Jumla ya gharama za miradi hiyo imefikia shilingi 1,448,140,672/=. Miongoni mwa vyanzo vya fedha, mfuko wa jimbo umechangia shilingi 13,325/=.
Miradi hiyo imejumuisha sekta za elimu ya msingi na sekondari, afya, miundombinu kupitia TARURA, utawala, pamoja na miradi ya TASAF.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Madaba, Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama, amewashukuru wananchi wa Kijiji cha Kipingo kwa mapokezi mazuri na ushirikiano wanaoonyesha katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Amesisitiza umuhimu wa mshikamano na ushirikiano wa wananchi katika kuleta maendeleo endelevu kwa jimbo lao.
Mhagama ameeleza kuwa ziara yake katika kijiji hicho inalenga kufanya tathmini ya maendeleo ya Jimbo la Madaba na kuhimiza wananchi kujitathmini kwa kina katika uchaguzi ujao ili kuchagua viongozi wenye uwezo wa kuleta maendeleo kwa wananchi wote.
Aidha, amewahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo za kijiji chao.
Katika hotuba yake, Mheshimiwa Mhagama amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa anazozifanya kuwaletea maendeleo wananchi wa Tanzania, hususan wa Jimbo la Madaba.
Pia amewasisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi ujao ili kuchagua viongozi wenye nia ya dhati ya kuendeleza maendeleo katika jamii na Taifa kwa ujumla.
Social Plugin