Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAWATAKA WALIMU KUEPUKA SIASA KAZINI

 Baadhi ya Walimu wa shule za Msingi na Sekondari Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma,wakiimba wimbo maalum wa mshikamo wakati wa Mkutano Mkuu wa Chama hicho uliofanyika katika Ukumbi wa St Kilian Mbinga

Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma Kisare Makori,akisalimiana na baadhi ya Viongozi wa Chama cha Walimu Tanzania(CWT)Wilaya kabla ya kufungua mkutano Mkuu wa  mwaka wa Chama hicho uliofanyika katika Ukumbi wa St Kilian Mbinga Mjini.

Mjumbe wa kamati ya utendaji  ya Chama cha Walimu Tanzania(CWT) anayewakilisha Mkoa wa Ruvuma Mwalimu Sabina Lipukila,akilishwa keki na Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Kisare Makori

Na Regina Ndumbaro - Mbinga. 

Serikali ya Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma imewataka walimu wa Wilaya hiyo kujiepusha na masuala ya siasa wanapokuwa kazini na badala yake wajikite katika kufundisha kwa kufuata sheria, kanuni, na miongozo ya elimu.

 Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa mwaka wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Mbinga, Mkuu wa Wilaya hiyo, Kisare Makori, amewasisitiza walimu kufanya kazi kwa bidii na kuepuka migogoro isiyo na tija. 

Ameeleza kuwa serikali inatambua mchango mkubwa wa walimu katika maendeleo ya taifa, hivyo inajitahidi kuboresha mazingira yao ya kazi na kuhakikisha wanapandishwa madaraja kwa wakati ili kuongeza ari ya utendaji kazi.

Mkuu wa Wilaya amewahimiza walimu kushirikiana na serikali katika sekta ya elimu kwa manufaa ya taifa na pia kujiendeleza kitaaluma ili kuendana na mahitaji ya sasa. 

Amebainisha kuwa serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imefanya juhudi kubwa kuboresha sekta ya elimu, ikiwa ni pamoja na kushughulikia changamoto zinazowakabili walimu. 

Aidha, amewataka walimu kuwa mabalozi wa maendeleo kwa kuhamasisha wananchi kushiriki katika uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kuchagua viongozi bora kwenye uchaguzi ujao wa Oktoba mwaka huu.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya na Halmashauri ya Mji Mbinga kutumia mapato ya ndani kulipa madeni ya walimu ili kuwawezesha kufanya kazi kwa bidii. 

Amesema malipo ya madeni hayo yataongeza motisha kwa walimu na kusaidia kuinua kiwango cha elimu kwa watoto mashuleni. 

Viongozi wa CWT Wilaya ya Mbinga, wakiongozwa na Katibu wa chama hicho, Chacha Maro, wamempongeza Rais Samia kwa kubadili muundo wa utumishi wa walimu, hatua iliyoongeza ukomo wa madaraja kulingana na viwango vya elimu, jambo ambalo limeleta faraja kwa walimu wengi.

Pamoja na mafanikio hayo, Chacha Maro ameeleza kuwa walimu bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo suala la kikokotoo cha pensheni ambacho kimekuwa kikwazo kwa wastaafu kupata mafao stahiki. 

Amesema wastaafu wanapokea fedha kidogo isiyokidhi mahitaji yao, hivyo ameiomba serikali ifanyie marekebisho mfumo huo. 

Changamoto nyingine aliyoitaja ni uhaba wa walimu na nyumba za walimu, hasa katika maeneo ya vijijini ambako hata nyumba za kupanga hazipatikani kwa urahisi, jambo linalowalazimu walimu kuishi mbali na vituo vyao vya kazi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CWT Wilaya ya Mbinga, Nicomdem Hyera, amewataka viongozi wa walimu katika shule mbalimbali kukusanya changamoto zinazowakabili walimu na kuzifikisha katika ngazi za juu ili zitatuliwe. 

Naye Afisa Elimu wa Mkoa wa Ruvuma, Judith Mpenzile, amesema mkoa huo bado uko nyuma kitaaluma, hivyo walimu wanapaswa kuongeza bidii katika ufundishaji ili kuinua kiwango cha elimu. 

Mkutano huo ulihudhuriwa na walimu wa shule za msingi na sekondari kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Mbinga.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com