Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SHYCOM ALUMNI WAKABIDHI MABWENI CHUO CHA UALIMU SHINYANGA

Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog

Wanafunzi wa chuo cha ualimu Shinyanga SHYCOM wametakiwa kuitunza miundombinu ya majengo ambayo imegharimu fedha nyingi ili iweze kudumu na kuleta tija kwa kuwawezesha kuwa katika mazingira mazuri ya kujifunzia.

Rai hiyo imetolewa Leo Machi 15, 2025 na Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya elimu Sayansi na Teknolojia Sebastian Inoshi wakati wa hafla fupi ya kukabidhi bweni la Uhuru na Jamhuri chuo cha ualimu Shinyanga yaliyofanyiwa ukarabati na Shycom Alumni Marathon ambao ni wanafunzi waliosoma katika chuo hicho.

"Juhudi hizi ni ishara halisi ya uzalendo na sisi tunapokea kwa mikono miwili ukarabati huu mlioufanya kwani maendeleo ya sekta ya elimu yanahitaji ushirikiano wa wadau wote hivyo natoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kuboresha mazingira ya kujifunzia kama ilivyofanywa na Shycom Alumni kupitia Shycom Alumni Marathon kutokana na jitihada hizi tutakuwa na elimu bora na kuzalisha wasomi wenye weledi",

"Pia nitoe rai kwa wanafunzi, walimu na wasimamizi kutunza miundombinu hii iliyokarabatiwa ili iweze kudumu kwa muda mrefu lakini pia serikali inaendelea kuboresha upatikanaji wa elimu kuanzia shule ya msingi Hadi vyuo", ameongeza Inoshi.

Awali akitoa taarifa ya ukarabati wa mabweni hayo Katibu wa kamati Shycom Alumni Marathon Josta Dominic amesema jumla ya Shilingi Milioni 124.2 zimetumika kukarabati mabweni hayo na miundombinu yake.

Mkurugenzi Msaidizi wa vyuo vya ualimu nchini Huruma Mageni amesema hatua ya kukarabati mabweni hayo kwa kukusanya fedha kwa wanafunzi ambao waliwahi kusoma katika chuo hicho ni jambo la kizalendo huku Mwakilishi wa kampuni ya Jambo Group Sarehe Mohamed akisema umoja na mshikamano ndiyo umefanikisha zoezi hilo.
Katibu wa kamati Shycom Alumni Marathon Josta Dominic akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mwakilishi wa kampuni ya Jambo Group Salehe Mohamed akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mkurugenzi Msaidizi wa vyuo vya ualimu nchini Huruma Mageni akizungumza kwenye hafla hiyo ya makabidhiano.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya elimu Sayansi na Teknolojia Sebastian Inoshi akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mkurugenzi Msaidizi wa vyuo vya ualimu nchini Huruma Mageni akizindua jengo la bweni la wanafunzi lililofanyiwa ukarabati kwenye hafla hiyo ya makabidhiano.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com