
Wafanyakazi wa Souwasa Manispaa Ya songea Mkoani Ruvuma wakionesha namna ya kupanda miti siku ya kilele cha wiki ya maji
Na Regina Ndumbaro Songea, Ruvuma.
Katika kuadhimisha Wiki ya Maji mwaka 2025, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Manispaa ya Songea (SOUWASA) imefanya zoezi la upandaji miti katika chanzo cha Bonde la Mto Ruhila.
Zoezi hili lina lengo la kuhifadhi vyanzo vya maji na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji safi kwa wakazi wa Manispaa ya Songea.
Kaimu Mkurugenzi wa SOUWASA, Maswe Nyamhangwa, akizungumza wakati wa zoezi hilo, amewataka wananchi kuepuka kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo ya vyanzo vya maji.
Ameeleza kuwa hatua hiyo inalenga kulinda mazingira na kuhakikisha vizazi vijavyo vinapata maji safi.
Pia, amesema kuwa serikali imetoa shilingi bilioni 2.8 kwa ajili ya fidia kwa wananchi wanaoishi karibu na vyanzo vya maji, ikiwa ni juhudi za kuimarisha uhifadhi wa mazingira.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Ufundi wa SOUWASA, Mhandisi Japhary Yahaya, amesema Bonde la Ruhila linazalisha asilimia 70 ya maji yanayotumiwa katika Manispaa ya Songea.
Amehimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika kutunza miti iliyopandwa na kuepuka shughuli zinazoharibu mazingira, kama kilimo karibu na vyanzo vya maji, ukataji miti ovyo, na uchomaji miti, ili kulinda vyanzo vya maji.
Maadhimisho ya Wiki ya Maji mwaka huu yalianza tarehe 16 Machi na yatafikia kilele tarehe 22 Machi 2025, yakibeba kauli mbiu inayosema "Uhifadhi wa Uoto wa Asili kwa Uhakika wa Maji."
Kauli mbiu hii inasisitiza umuhimu wa utunzaji wa mazingira kama njia ya kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa jamii.
SOUWASA imepanga kuendelea na juhudi za upandaji miti katika maeneo mengine muhimu, ikiwemo Bonde la Luhira, ili kuimarisha uhifadhi wa mazingira.
Hatua hii inalenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji na kuhakikisha wakazi wa Manispaa ya Songea wanaendelea kupata maji safi kwa matumizi ya kila siku.



Social Plugin