
Wafanyakazi wa SOUWASA wakitoa elimu kwa mwananchi na mkazi wa Ruhuwiko Shuleni kuhusu umuhimu wa matumizi ya maji na kutumia fursa iliyotolewa bure ya kurejeshewa maji.

Wafanyakazi wa SOUWASA Songea wakizungumza na wananchi kuhusu huduma hiyo ya maji kwa kurejeshewa bila fidia yoyote
Na Regina Ndumbaro, Ruvuma
Katika kuelekea kilele cha Wiki ya Maji, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA) imezindua kampeni maalumu ya kuhamasisha wateja waliositishiwa huduma kurejesha maji yao kwa kulipa nusu ya deni lao.
Kampeni hii inalenga kuwapa fursa wakazi wa Manispaa ya Songea kurejesha huduma zao kwa urahisi, huku ikihamasisha jamii kuhusu umuhimu wa maji safi na salama.
Timu maalumu ya SOUWASA, ikiongozwa na Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja, Bi Baby Biko, imetembelea maeneo ya Ruhuwiko Kanisani na Ruhuwiko Shuleni ili kutoa elimu na kuwaeleza wananchi kuhusu ofa hii maalumu.
Timu hiyo imepita nyumba kwa nyumba kuhakikisha kila mkazi anayehitaji kurejesha huduma za maji anapata taarifa sahihi na fursa ya kufanikisha hilo kwa urahisi.
Ofa hii maalumu inatoa nafasi kwa wateja waliositishiwa huduma kurejeshewa maji bila fidia yoyote, endapo watalipa nusu ya deni lao ndani ya muda uliopangwa.
Kampeni hii itadumu kwa wiki moja, kuanzia tarehe 16 hadi 22 Machi 2025, na imelenga kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Songea wanaokabiliwa na deni la maji.
SOUWASA inawataka wakazi wa Manispaa ya Songea kuchangamkia fursa hii kwa haraka ili kuepuka usumbufu wa ukosefu wa maji katika makazi yao.
Huduma ya maji ni hitaji la msingi kwa kila kaya, hivyo mamlaka hiyo imeamua kuweka mazingira wezeshi kwa wateja wake ili waendelee kupata huduma bora kwa gharama nafuu.
Kampeni hii ni sehemu ya juhudi za SOUWASA kuhakikisha kila mkazi wa Songea anapata maji safi na salama kwa matumizi ya kila siku.
Mamlaka hiyo inaendelea kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa kulipa bili zao kwa wakati ili kuepusha usitishaji wa huduma na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji kwa wote.
Social Plugin