Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),litaendelea na utekelezaji wa miradi ya uzalishaji, usafirishaji, na usambazaji umeme, ikiwa ni pamoja na miradi ya Malagarasi, Kakono, Ruhudji, na Rumakali,kwa lengo la kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi .
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo (TANESCO), Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga, ameeleza hayo March 26,2025 Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwelekeo wa Shirika hilo chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita.
Amesema kuwa hali ya uzalishaji wa umeme nchini inaendelea kuimarika, na hadi Februari 2025, uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme kwenye gridi ya Taifa umefikia MW 3,796.71, huku mahitaji ya juu ya umeme yakiwa ni MW 1,908.
Mhandisi Nyamo-Hanga ameeleza kuwa mwaka 2021, uwezo wa uzalishaji wa umeme ulifikia MW 1,573.65, na kwamba kumekuwepo na maendeleo makubwa katika miradi mbalimbali ya uzalishaji.
"Mfano Mradi wa JNHPP, unatarajiwa kuongeza umeme MW 2115 kwenye gridi ya Taifa ifikapo Mei 2025, baada ya kumalizika kwa mitambo yake yote tisa. Hadi sasa, jumla ya mitambo 8 kati ya 9 za JNHPP zimeanza kuzalisha umeme, " amesema.
Ameongeza kuwa mradi wa JNHPP umefikia asilimia 99.82 ya utekelezaji, huku mradi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka JNHPP hadi Chalinze kwa msongo wa kilovoti 400, yenye urefu wa kilomita 160, ukiwa umefikia asilimia 99.75. Ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Chalinze, ambacho ni sehemu muhimu ya mradi huu, umefikia asilimia 97.59.
Mhandisi Nyamo-Hanga amegusia mafanikio mengine katika miradi ya uzalishaji umeme kwa kutumia maji na gesi asilia. Alieleza kuwa mradi wa Rusumo umefikia asilimia 99.9 na tayari unatoa MW 26.7 kwa gridi ya Taifa, huku mradi wa Kinyerezi I Extension ukiwa umefikia asilimia 98 na tayari unachangia MW 160.
"Tanzania inatarajiwa kunufaika na miradi ya umeme wa jua inayotekelezwa katika wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga,katika upande wa miundombinu ya usafirishaji umeme, urefu wa njia kuu za kusafirisha umeme umeongezeka kutoka kilomita 6,423.53 mwaka 2021 hadi kilomita 8,141.38 mwaka 2025, ikiwa ni ongezeko la asilimia 27,"ameeleza
Amesema hali hiyo inatoa picha ya maendeleo katika ufanisi wa miundombinu ya gridi ya Taifa na kwamba Tanzania imefanikiwa kuunganisha gridi za umeme za Kenya na Tanzania kupitia mradi wa Kituo cha Kupoza na Kusafirisha Umeme cha Lemuguru kilichopo Arusha.
"Utekelezaji wa miradi ya njia za kusafirisha umeme kutoka Morogoro hadi Dodoma na Iringa hadi Sumbawanga unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miaka michache ijayo, na kwamba Tanzania itajiunga na mtandao wa Gridi ya Umeme wa Jumuiya ya Nishati katika Ukanda wa Kusini mwa Afrika (SAPP),"amesema.
Pamoja na mambo mengine ameeleza kuwa miradi hiyo itakuwa na manufaa makubwa kwa uchumi wa nchi na kwa nchi za jirani.
"Katika kuunganisha mikoa mbalimbali ya Tanzania kwenye gridi ya Taifa,Kwa mfano, mkoa wa Kigoma umeunganishwa kwenye gridi ya Taifa kupitia Kituo cha Nyakanazi, huku mikoa ya Lindi na Mtwara pia ikitarajiwa kuunganishwa kwenye gridi hiyo kwa kupitia miradi mbalimbali ya usafirishaji umeme, "ameeleza.
Mkurugenzi Mkuu huyo ameeleza kuwa shirika limefanikiwa kuunganisha wateja wapya 5,394,168 katika kipindi cha kuanzia 2021 hadi 2025, huku idadi ya transfoma zilizotumika kusambaza umeme ikiongezeka kutoka 26,165 hadi 33,108.
Amesema kuwa idadi hii ya wateja ni ishara ya mafanikio katika upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi.
Social Plugin