Na Dotto Kwilasa, Dodoma
MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania(TRC), Masanja Kadogosa amewatoa hofu wafanyabiashara wakubwa wa usafirishaji mizigo kwa njia ya maroli kutokana na ujio wa reli ya kisasa ya mizigo ya mwendo kasi kuwa reli hiyo haiwezi kuua biashara yao bali itawanufaisha zaidi wafanyabiashara na mlaji wa mwisho.
Kadogosa ameyasema alipokuwa akitoa taarifa ya mafanikio ya miaka minne ya Shirika hilo katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan katika ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO Jijini Dodoma.
Kadogosa amezungumza hilo baada ya mwandishi wa habari kuuliza swali juu ya kuwepo kwa wasiwasi inayotokana na wafanya biashara hususani wasafirishaji wa mizigo kwa kutumia maroli kuwa uwepo wa reli hiyo inaweza kuua biashara ya wasafirishaji wa mizigo wanaotumia maroli.
Amesema hakuna uhusiano wowote wa kuua biashara ya wafanyabiashara ya maroli bali ujio wa reli ya mwendo kasi ya kusafirisha mizigo itakuwa mkombozi kwa wafanyabiashara wenyewe na mlaji wa mwisho kwa kupata mzigo kwa haraka na kuusafirisha muda mfupi.
Akitolea mfano wa vifaa vya ujenzi amesema watu wa Dar es Salaam wanaweza kununua saruji mfuko mmoja kwa Sh. 15,000 hadi 16,000 lakini mtu wa Kanda ya Ziwa ananunua kwa Sh.24000 hadi 26000 na hiyo inatokana na muda mrefu na gharama za njiani kwa njia ya barabara.
Amesema iwapo itatumika njia ya reli ya mwendo kasi itapunguza muda wa usafirishaji na gharama za njiani na kupelekea mnunuzi huyo kununua saruji kati ya Sh. 18000 hadi 20000 hivyo kujikuta anaokoa kati ya Sh. 4000 au 6000 jambo ambalo ni mafanikio makubwa kwa mlaji wa mwisho.
Mafanikio mengine ya Shirika hilo ni pamoja na utekelezaji wa ahadi ya Rais Samia ya kuendeleza mradi huo na sasa umejumuisha, kipande cha Isaka – Mwanza, Makutopora-Tabora, Tabora – Isaka na kisha kumalizia vipande vya awamu ya pili kuelekea Kigoma.
Ameeleza Kadogosa kuwa wakati Serikali ya Awamu ya Sita inaingia madarakani, ujenzi wa mradi wa SGR ulikuwa ukitekelezwa katika vipande viwili vya Dar es salaam hadi Morogoro ambapo utekelezaji wake ulikuwa umefikia asilimia 83.55 na Morogoro hadi Makatupora ulikuwa umefikia asilimia 57.57.
“Mnamo Juni 2024, vipande hivi kutoka Dar es Salaam hadi Makutopora vyenye urefu wa kilometa 722 vimekamilika na kuanza kutoa huduma za usafirishaji wa abiria.
“Mafanikio makubwa ambayo Shirika kupitia serikali ni kuona umuhimu wa kuunganisha nchi za jirani kwa mtandao wa reli jambo ambalo limakuza uchumi zaidi na kuendelea kukuza mahusiano kato ya nchi ya Tanzania na nchi jirani,” amesema.
Social Plugin