Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imeendelea kufanikisha utoaji wa vifaa vya TEHAMA kwa shule na walimu, ikiwemo kompyuta, projecta na vifaa vingine vya kisasa.
Aidha jumla ya shule 1,121 zimepewa vifaa hivi, na walimu 3,798 wamepatiwa mafunzo ya TEHAMA ili kuboresha ufundishaji na ujifunzaji katika shule za umma.
Hayo yameelezwa leo Jijini Dodoma na Afisa Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Mhandisi Peter Mwasalyanda wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa mfuko huo kwa Kipindi cha miaka minne.
"Mradi mwingine muhimu wa UCSAF ni kuboresha usikivu wa Redio ya Taifa ya TBC, ambapo vifaa 19 vya kurushia matangazo vimejengwa na ruzuku ya TZS 6.27 bilioni,lengo ni kuhakikisha kuwa matangazo ya TBC yanapata usikivu mzuri nchi nzima, hasa katika maeneo ya vijijini,"ameeleza.
Kwa upande mwingine, amesema UCSAF imeendelea kuhamasisha matumizi ya TEHAMA kwa wasichana, kupitia maadhimisho ya Siku ya Wasichana na TEHAMA, ambapo mafunzo yanatolewa kwa wanafunzi wa kike ili kuwaandaa kwa masomo ya sayansi na teknolojia.
"Kazi hii ya maendeleo ya miundombinu ya mawasiliano, hasa katika maeneo ya vijijini, inaonekana kuwa na manufaa makubwa kwa maendeleo ya taifa, na UCSAF inaahidi kuendeleza juhudi zake ili kuhakikisha kwamba kila mtanzania anapata huduma bora za mawasiliano, "amesisitiza.
Licha ya hayo ameeleza kuwa UCSAF mejizatiti kufikisha huduma za mawasiliano kwenye kata 1,974 na vijiji 5,102 nchini ambapo hadi sasa, minara 2,152 ya mawasiliano imejengwa, ambayo imewanufaisha zaidi ya wakazi milioni 29.
Mtendaji huyo ameeleza kuwa, Serikali kupitia UCSAF imewekeza katika miradi mikubwa ya ujenzi wa minara ya mawasiliano vijijini, ikiwa ni pamoja na mradi wa minara 758 ambao unatarajiwa kufikia kata 713, wilaya 127, na mikoa 26. Hadi Machi 2025, minara 430 imeshakamilika na tayari inatoa huduma.
Amesema Mradi huo umetumia ruzuku ya TZS 126 bilioni, na unatarajiwa kutoa huduma kwa wananchi takribani milioni 8.5.
"Tumefanya kazi kubwa katika kuboresha huduma za mawasiliano nchini Tanzania, hasa kwa kuhakikisha kwamba huduma hizo zinawafikia wananchi hata katika maeneo ya vijijini,hii ni sehemu ya juhudi za serikali katika kuimarisha miundombinu ya mawasiliano, kwa kufuata malengo ya Rais Samia Suluhu Hassan,"ameeleza.
Amesema kuwa, tangu kuanzishwa kwa mfuko huo kwa sheria ya Bunge namba 11 ya mwaka 2006, umetekeleza miradi mingi ya kimaendeleo katika sekta ya mawasiliano ikiwemo juhudi ya kuboresha huduma za intaneti kwa kupitia ujenzi wa mtandao wa Wi-Fi bure katika maeneo mbalimbali ya umma.
"Hadi sasa, jumla ya maeneo 7 yamefungwa na Wi-Fi bure, huku serikali ikitarajia kuongeza idadi hiyo katika maeneo mengine 17," amesema
Social Plugin