Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

USAMBAZAJI UMEME WAFIKIA ASILIMIA 98 NJOMBE

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imehitimisha ziara ya siku tatu mkoani Njombe kwa kukagua utekelezaji wa miradi ya Nishati Vijijini (REA) inayotekelezwa na serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO). Kwa upande wa REA ziara hiyo imehitimishwa katika kijiji cha Welela, Jimbo la Lupembe, na kisha kupongeza juhudi zinazofanywa na Serikali kuhakikisha umeme unawafikia wananchi wa vijijini kwa kasi inayostahili.


Akizungumza wakati wa hitimisho la ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Dkt. David Mathayo, alisema kamati yake imeridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo, lakini akasisitiza kuwa bado kuna haja ya kuongeza kasi ili kufanikisha lengo la Serikali la kuhakikisha vitongoji vyote nchini vinaunganishwa na gridi ya taifa kwa wakati.


Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha changamoto zote za umeme vijijini zinatatuliwa kwa haraka ili kuboresha maisha ya wananchi.


"Serikali inatambua umuhimu wa umeme kwa maendeleo ya wananchi, hususan katika sekta za elimu, afya, na biashara. Tutaendelea kuweka msukumo ili kuhakikisha vitongoji vyote vinapata umeme kwa wakati, na kwa hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi," alisema Mhe. Kapinga.


Wananchi wa vijiji mbalimbali kikiwemo Welela, wameeleza furaha yao kwa kufikishiwa umeme ambapo wamesema hatua hiyo imewasaidia kuondokana na changamoto ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma muhimu, ikiwemo mashine za kusaga nafaka.


Mkurugenzi wa wakala nishati Vijijini (REA), Mhandisi Jones Olotu, ameeleza kuwa jumla ya shilingi bilioni 81.6 zinatumika kutekeleza miradi ya usambazaji wa umeme vijijini mkoani Njombe na kwamba miradi hiyo ni sehemu ya mpango wa kitaifa wa kuhakikisha vijiji vyote vinaunganishwa na umeme.

Ziara hiyo kwa upande miradi ya REA imehitimishwa kwa Kamati ya Bunge kupokea taarifa rasmi ya utekelezaji wa miradi ya umeme mkoani Njombe ambapo miradi inayotekelezwa na REA Mkoani Njombe inagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 81.6

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com