Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANANCHI WA KATA YA MISECHELA NA NAMASAKATA WAMSHUKURU RAIS SAMIA KWA MAENDELEO

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho akizungumza na wananchi na wanachama kata ya Namasakata wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma

Na Regina Ndumbaro - Tunduru. 

Wananchi wa Kata ya Misechela na Namasakata, wilayani Tunduru, wameeleza pongezi zao kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake katika kuwaletea maendeleo. 

Katika ziara ya Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho, wananchi hao wamesema kuwa serikali ya awamu ya sita imekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza Ilani ya CCM kwa vitendo, hasa katika sekta za kilimo, afya, elimu, na miundombinu.

Bi Asha Hamad, mkazi wa Kata ya Namasakata, ameeleza kuwa kupitia mpango wa pembejeo za ruzuku, maisha yake na ya familia yake yameimarika kwa kiasi kikubwa. 

Amefafanua kuwa kabla ya msaada huo, alikuwa hana uwezo wa kumudu baadhi ya mahitaji muhimu, lakini sasa ameweza kunufaika na kilimo cha korosho na kuboresha maisha ya familia yake, ikiwa ni pamoja na kumudu samani bora kama vitanda na magodoro mazuri. 

Amesisitiza kuwa hatua hii ni ushahidi wa namna serikali inavyowajali wakulima wadogo kwa kuwapa nyenzo za kuboresha uzalishaji wao.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho, amewahimiza wanachama wa chama hicho kuendelea kuiunga mkono serikali ya Dkt. Samia kwa kazi kubwa inayoendelea kufanyika. 

Ameeleza kuwa maendeleo katika sekta ya umeme, barabara, afya na elimu yanadhihirisha dhamira ya dhati ya serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora. 

Aidha, amewapongeza wananchi wa kata hizo kwa ushindi mkubwa waliopata katika uchaguzi uliopita, huku akisisitiza kuwa maeneo yaliyoshindwa yalitokana na changamoto za kiuongozi ambazo zinapaswa kutafutiwa suluhisho.

Katika mkutano huo, Mwenyekiti huyo amewakumbusha wanachama wa CCM kuhusu utaratibu wa kugombea nafasi mbalimbali ndani ya chama.

 Amesema kuwa kila mwanachama anayehisi ana sifa za kugombea anapaswa kufuata taratibu rasmi kwa kuchukua fomu za maombi na kushiriki kwenye mchakato wa uteuzi kwa mujibu wa kanuni za chama. 

Amesisitiza umuhimu wa viongozi wa chama kudumisha nidhamu, kuzingatia miiko na maadili ya chama, na kuepuka upendeleo ili kuhakikisha mshikamano na umoja ndani ya chama.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM Wilaya ya Tunduru, Yusuf Hassan Mabena, amejibu maswali mbalimbali kutoka kwa wananchi wa Namasakata, hasa kuhusu madai ya unyanyasaji wa wanachama. 

Amekanusha tuhuma hizo kuhusu  kwamba kuna watu wanaotumwa na viongozi wa wilaya kwa lengo la kuwabagua wanachama, na akawasihi wananchi kuwa makini na taarifa zisizo na ukweli. 

Pia, amewahakikishia kuwa chama na serikali wataendelea kushirikiana kwa karibu katika kuhakikisha kila mwananchi anapata haki zake bila upendeleo au ubaguzi.


Wananchi wa Kata ya Namasakata

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com