Habari Mpya

    Loading......

WANANCHI WA TUNDURU WAOMBA SALFA ILETWE MAPEMA KWA AJILI YA KILIMO CHA KOROSHO

Wananchi na wanachama waliojitokeza kumsikiliza Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho katika ziara yake ya kata kwa kata katika Wilaya ya Tunduru
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho akizungumza na wananchi na wanachama wa CCM katika kata ya Nandembo Wilayani Tunduru

Wananchi na wanachama wa CCM kata ya Nandembo wakimsikiliza Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa Oddo Mwisho pichani hayupo katika ziara yake ya kata kwa kata yenye lengo la kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi na wanachama hao



Mwenyekiti Wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa Oddo Mwisho pichani akisalimiana na baadhi ya wananchi na wanachama katika kata ya Nampungu Wilaya ya Tunduru


Na Regina Ndumbaro Tunduru. 

Wananchi wa kata za Nandembo, Nampungu, na Kidodoma katika Wilaya ya Tunduru wamemuomba Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho, kufikisha malalamiko yao kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu upatikanaji wa salfa kwa wakati. 

Wakulima hao, akiwemo Rehema Malipesa na Saidi Hashimu Mkwekwele, wamesema pembejeo hizo ni muhimu kwa mafanikio ya kilimo cha korosho na wameomba serikali kuhakikisha wanazipata mapema ili kuepuka ucheleweshaji wa kuandaa mapema zao hilo.

Mbali na suala la salfa, wananchi hao pia wamemweleza Mwenyekiti Oddo Mwisho kuhusu hitaji la kuwa na ofisi ya ushirika AMCOS katika kata yao. 

Wamesema ofisi hiyo itawasaidia wakulima wa korosho kuepuka kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya shughuli za kibiashara. 

Pamoja na changamoto hizo, wananchi wametoa pongezi kwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia pembejeo ambazo zimewasaidia kunufaika na kilimo cha korosho.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tunduru, Hailu Mussa,amejibu maswali ya wananchi  kuwa serikali inatambua changamoto zinazowakabili wakulima wa korosho na inaendelea kufanya jitihada kuhakikisha pembejeo zinawafikia kwa wakati. 

Amesema hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa ili kuboresha sekta ya kilimo, na serikali itaendelea kushirikiana na wakulima ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo muhimu.

Katika ziara yake kwenye kata za Nandembo, Nampungu, na Kidodoma, Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Oddo Mwisho, amezungumzia maendeleo yaliyofanyika katika maeneo hayo. 

Ameeleza kuwa licha ya miundombinu ya barabara kuwa mibovu, serikali inaendelea kuchukua hatua za kuboresha hali hiyo. 

Pia amewahakikishia wananchi kuwa serikali inafanya kazi kuhakikisha huduma muhimu kama maji safi, umeme, afya, na elimu zinawafikia wananchi wote.

Mwenyekiti huyo amesisitiza kuwa serikali ya CCM ina dhamira ya kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka wa fedha 2025/26, umeme utakuwa umewafikia wananchi wa vitongoji vyote.

 Pia ameeleza kuwa uboreshaji wa miundombinu utaongeza fursa za maendeleo kwa wananchi.

 Amewataka wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali na kushiriki kwa wingi katika uchaguzi mkuu ujao. 

Pia amemsifu Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini Mheshimiwa Hassan Kungu, kwa kusikiliza na kushughulikia changamoto za wananchi wake, hususan katika sekta ya miundombinu ya barabara ambapo tayari mkandarasi amepatikana kwa ajili ya kutekeleza mradi wa barabara kutoka Nandembo hadi Nampungu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com