Na Lydia Lugakila - Bukoba
Wananchi katika Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera wametakiwa kutokutunza taka katika kaya zao na maeneo mbali mbali ya biashara kwani kwa kufanya hivyo ni hatari kwa afya zao huku watakaobainika kuchukuliwa hatua za kisheria.
Kauli hiyo imetolewa na Mganga Mkuu wa Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera Dkt. Peter Mkenda wakati Akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake waliotaka kujua masuala mbali mbali yahusuyo afya ndani ya Manispaa hiyo.
Mkenda amesema Manispaa hiyo imeweka utaratibu mzuri wa ukusanyaji wa taka katika mitaa ambapo magari yanapaswa kuzoa taka licha ya wananchi kutokutoa taka hizo kwa wakati.
"Taka hazipaswi kukaa kwenye kaya au eneo la biashara zaidi ya masaa 48 yakizidi masaa 48 zinaanza kuoza na zinatoa harufu mbaya zinavuta wadudu waenezao magonjwa na kuleta hatari zaidi",amesema Mkenda.
Amewasihi wananchi kupeleka taka kwenye magari ya kuzoa taka kwa mujibu wa sheria.
Ameongeza kuwa wao kama wataalam wa Afya kwa kutumia sheria ya Afya ya jamii ya mwaka 2009 wakimkamata mwananchi au mfanyabiashara anayerundika taka zaidi ya masaa 48 atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Aidha amesema kwa ushuru wa taka ambao Manispaa imeweka kwa utaratibu waendelee kulipa ushuru wa taka ambayo ni fedha isiyozidi shilingi elfu 2,000 kwa mwezi.
Mganga mkuu huyo amewashauri Wananchi kuendelea kulipa ushuru wa taka ikiwemo kuzitoa kwenye kaya zao wasibaki nazo kwani ni chanzo Cha magonjwa.
Amesema katika kipindi hiki cha mvua mito mikubwa na midogo imejaa hivyo Wananchi waendelee kuzingatia kanuni za Afya hasa kukwepa matumizi ya maji ambayo yapo katika vyanzo ambavyo siyo sahihi.
"Mito inabeba uchafu wa kila aina unaotoka katika maeneo mbali mbali wapo wanaofulia nguo zao mtoni, wanaotililisha majitaka yatokayo kwenye vyoo hadi kwenye mito hivyo inakuwa ni chanzo cha magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindu pindu", amesema mtaalam huyo wa Afya.
Hata hivyo amesema kuwa kwa historia ya nyuma na hata mwaka huu kipindi cha mvua nyingi Wananchi hupata magonjwa mengi yakiwemo ya kuharisha na kutapika ambapo ni viashiria vya ugonjwa wa kipindu pindu.
Amewasihi wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kwa kipindi hiki ikiwemo kunywa maji yaliyochemshwa,kutumia maji ya bomba, kula vyakula vya moto, matumizi sahihi ya vyoo, kunawa mikono mara mara mara kwa maji tiririka ili kuepukana na magonjwa mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuendelea kufuatilia taarifa mbali mbali za kiafya katika tovuti za wizara ya afya pia na vyombo vya habari.
Social Plugin