Na Mwandishi wetu,Dodoma
Jumla ya watoto 54 waliozaliwa wakiwa hawasikii wamepandikizwa vifaa vya kuwasaidia kusikia Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) katika kipindi cha miaka minne ya utekelezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dkt. Samial Suluhu Hassan na kufanya idadi ya walionufaika kufikia 88 tangu kuanzishwa huduma hii nchini Juni 2017.
Akitoa taarifa ya mafanikio ya MNH ya kipindi tajwa, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji Dkt. Rachel Mhaville aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo amesema, Serikali imewagharamia watoto hao 54 kila mmoja TZS. 45 Mil sawa na TZS. 2.43 Bil, endapo wangeenda kutibiwa nje ya nchi Serikali ingelipa TZS. 120 Mil kwa kila mtoto sawa na TZS. 6.5 Bil. hivyo kuokoa kiasi cha TZS. 4 Bil. Tanzania ni nchi ya kwanza kutoa huduma hii kupitia hospitali za umma katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki” amesema Dkt. Mhaville.
Kuhusu huduma ya kibingwa ya kupima kiwango cha kusikia kwa watoto wachanga, amefafanua kuwa katika kipindi cha miaka minne iliyopita hospitali imefanikiwa kuanzisha huduma ya ubingwa bobezi wa kupima watoto wachanga kiwango cha kusikia mara tu wanapozaliwa ili kugundua mapema na kutoa matibabu ambapo tangu kuanzishwa kwa huduma hii mwishoni mwa mwaka 2023 tayari watoto wachanga 320 wamenufaika na waliobainika kuwa na shida hiyo wamewekwa kwenye mpango maalum wa ufuatiliaji ikiwemo mafunzo ya kuongea na baadaye kupandikizwa vifaa vya kuwasaidia kusikia.
Pia katika kukabiliana na tatizo la watoto la kutokusikia mwaka 2023, Serikali ilianzisha maabara ya kimataifa ya umahiri ya upasuaji na upandikizaji vifaa vya kusaidia kusikia kwa watoto na kuifanya kuwa nchi ya kwanza Kusini mwa Jangwa la Sahara kuwa na maabara hiyo. Hadi sasa madaktari wazawa 36 na wengine 18 kutoka Kenya, Uganda, Rwanda, Ethiopia, Nigeria na Ghana wamepatiwa mafunzo hayo kupitia maabara hiyo
Aidha katika kipindi tajwa hospitali imefanikiwa kuzindua mtambo unaotumia tiba hewa yenye mgandamizo wa oksijeni kwa asilimia 100 ambao unatibu magonjwa zaidi ya 10, hivyo Tanzania ni nchi ya kwanza katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na ya pili Kusini mwa Jangwa la Sahara kupitia Hospitali za Umma kutumia mtambo huo uliogharimu TZS. 250Mil.
Hadi sasa wagonjwa 54 wamenufaika na huduma hiyo na kupona magonjwa mbalimbali ikiwemo vidonda sugu, maumivu makali ya mgongo na wagonjwa waliopata madhara ya mionzi tiba ya saratani.
Social Plugin