
Na Regina Ndumbaro - Songea.
Project Healthy Children Tanzania Limited imeanza kufunga mashine maalum za kusaga nafaka zenye uwezo wa kuchanganya virutubishi kwenye chakula katika Mkoa wa Ruvuma, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupambana na udumavu kwa watoto walio chini ya miaka mitano, pamoja na matatizo ya kiafya kama mgongo wazi na upungufu wa damu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Mahusiano na Serikali wa Sanku, Gwao Omari Gwao, amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa kampuni hiyo nchini mwaka 2015, wamefanikiwa kufikia mikoa 26 na halmashauri 157, wakiwa na lengo la kueneza teknolojia hiyo hadi kila kijiji nchini.
Kwa sasa, mkoani Ruvuma kuna wazalishaji 36 wanaotumia teknolojia ya Sanku katika urutubishaji wa nafaka, na mafanikio hayo yamechangiwa na mashirikiano mazuri kati ya serikali na kampuni hiyo.
Gwao ameeleza kuwa mashine hizo huchanganya virutubishi muhimu kama madini ya chuma, asidi ya foliki, zinki, na vitamini, ambavyo vina mchango mkubwa katika kuimarisha afya ya wananchi, hasa watoto na wajawazito.
Ameongeza kuwa serikali imekuwa ikitoa elimu na kutengeneza sera rafiki zinazosaidia utekelezaji wa mradi huo.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Maendeleo ya Biashara wa Sanku, Christian Lutaja, amesema kuwa zaidi ya mashine 36 zimefungwa katika Mkoa wa Ruvuma pekee, huku wazalishaji wakionyesha mwitikio mkubwa kutokana na manufaa ya teknolojia hiyo.
Mfanyabiashara mmoja, Gaddaf Mgomi, ameeleza kuwa tangu apate mashine hiyo, wateja wake wameongezeka kutoka 25 hadi 100 kwa siku, hasa kutokana na ongezeko la uelewa kuhusu virutubishi miongoni mwa shule na jamii kwa ujumla.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dkt. Lois Chamboko, amesema kuwa hali ya lishe bado ni duni katika mkoa huo, kulingana na takwimu za utafiti wa mwaka 2022.
Amebainisha kuwa udumavu uko kwenye asilimia 35.6, uzito pungufu asilimia 12.2, upungufu wa damu kwa watoto asilimia 45, na kwa wajawazito asilimia 30.
Amesisitiza kuwa uwekezaji kama huu wa Sanku ni muhimu sana katika kusaidia kubadili hali hiyo ya lishe.
Social Plugin