Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MKUU WA WILAYA YA MASASI APONGEZA HUDUMA BORA ZA AFYA HOSPITALI YA MKOMAINDO


Mkuu wa Wilaya ya Masasi Rechal Kassanda akiwa katika wodi ya akina mama wajawazito na watoto Hospitali ya Mkomaindo Wilayani Masasi wakati wa ziara yake
Mkuu wa Wilaya ya Masasi Rechal Kassanda akisaini Daftari la wageni Katika Hospitali ya Mkomaindo Wilayani Masasi.
Wauguzi na Madaktari wa Hospitali ya Mkomaindo wilayani Masasi
Mkuu wa Wilaya ya Masasi Rechal Kassanda akitoka ndani ya jengo la Hospitali ya Mkomaindo alipotembelea katika ziara yake Hospitali hapo
Mkuu wa Wilaya ya Masasi Rechal Kassanda akiwa katika ziara yake Hospitali ya Mkomaindo baada ya kukabidhiwa Majukumu yake na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo

Na Regina Ndumbaro - Masasi. 

Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Mheshimiwa Rachel Kassanda, ameipongeza Hospitali ya Mkomaindo iliyopo Masasi Mjini kwa kutoa huduma bora kwa wananchi. 

Pongezi hizo amezitoa wakati wa ziara yake rasmi hospitalini hapo, ikiwa ni moja ya shughuli zake za mwanzo tangu kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa Mkuu wa Wilaya ya Masasi.

Katika ziara hiyo, Rachel ameeleza kufurahishwa kwake na hali ya usafi pamoja na huduma zinazotolewa hospitalini hapo. 

Amesema ameshuhudia mazingira safi na huduma zenye viwango, jambo linaloonesha juhudi na moyo wa kujituma kwa watumishi wa afya. 

“Nimeridhishwa sana na huduma mnazozitoa hospitalini hapa, mko vizuri sana katika suala la usafi. Hongereni sana,” amesema.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ametumia fursa hiyo kuwafariji wagonjwa waliolazwa hospitalini kwa kuwapa zawadi mbalimbali. 

Zawadi hizo zilijumuisha sabuni za kufulia, juisi, mataulo ya wanawake, na sabuni za kuogea. 

Walengwa wakuu walikuwa wanawake wajawazito pamoja na wale waliokuwa tayari wamejifungua, ikiwa ni ishara ya upendo na kutambua changamoto wanazopitia.

 Rachel amewataka wahudumu wa afya katika hospitali hiyo kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi wote. 

Amesisitiza umuhimu wa kutunza siri za wagonjwa, kuwa na huruma, na kufuata maadili ya kazi yao kwa weledi. 

Amesema serikali inategemea huduma bora kutoka kwao ili kuhakikisha jamii inapata huduma stahiki.

Kwa upande wa watumishi wa Hospitali ya Mkomaindo wamemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kutembelea hospitali yao na kutambua mchango wao katika sekta ya afya. 

Wameeleza kuwa ujio wake umewatia moyo na kuwahamasisha kuongeza bidii katika kuwahudumia wananchi, huku wakiahidi kuendeleza jitihada za utoaji huduma bora

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com