Na Mwandishi Wetu - Dar es salaam
WAJUMBE wa Kamati ya Ustawi wa jamii ya Baraza la wawakilishi Zanzibar wametembelea Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kwa lengo la kujifunza ili waweze kuishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayolenga kujenga Chuo cha mabaharia kwa upande wa Zanzibar.
Akizungumza mara baada ya kutembelea mitambo na vifaa vya kujifunzia na kujifundishia Mwenyekti wa Kamati hiyo Mhe. Sabiha FilFil Thani amesema anaushukuru uongozi wa Chuo kwa ushirikiano waliotoa.
"Tumefanikiwa kujifunza kuhusu namna ya kuendesha Chuo cha Bahari lakini pia kujipanga kuwa na vifaa vya mafunzo vitakavyowezesha kutoa elimu bora pamoja na taaluma kwa wakufunzi watakaotarajiwa kuwa wakufunzi wa chuo hicho" amesema.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya amali Zanzibar Mhe. Ali Abdul-Gulam Hussein amesema ziara hiyo imekuwa ya umuhimu mkubwa kwa kutembelea Chuo cha DMI ambacho kimetangulia katika taaluma za ubaharia.
"Hii itawasaidia kuepuka makosa wakati wa ujenzi wa chuo kipya lakini pia kuishauri Serikali ipasavyo hususani katika eneo la vifaa vya kujifunzia ambavyo vina gharama kubwa itakayolazima Serikali kuwekeza fedha nyingi" amesema.
Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam Prof. Tumaini Gurumo amesema kuwa chuo kimefanikiwa kuwaeleza shughuli zinazofanyika hasa eneo la kozi za ubaharia zinazosimamiwa na mikataba ya Kimataifa unaojulikana kama STCW 1978.
Amesema kozi hiyo inalazimu Chuo kuwa na Wakufunzi wabobezi Mabaharia, vifaa vya kujifundishi vinavyojulikana kama Simulators ambazo ni nusu ya uhalisia wa baharini na wanafunzi wa ubaharia kufanya mazoezi ya uhalisia baharini.
Ameongeza kuwa Chuo cha bahari DMI kinasimamiwa na taasisi za Kimataifa na Kitaifa, ambapo Kimataifa DMI inasimamiwa na taasisi iliyothibitishwa na shirika la Kimataifa la Bahari IMO inayojulikana kama DNV inayotazama viwango vya ubora vya elimu vinavyotolewa chuoni na Kitaifa Chuo kinasimamiwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa kupande wa mitaala inayotolewa kwa mabaharia.
“Katika kukidhi matakwa ya kitaifa na kimaifa chuo tumefanikiwa kuongeza mitambo ya kisasa ya kujifunzia na kufundishia inayolenga kuhakikisha viwango vya ubora vya elimu vinavyoendana na teknolojia ambapo itawalazimu chuo tarajiwa cha Zanzibar kufuata matakwa hayo. Alisema Prof Tumaini.
Chuo cha DMI ni chuo pekee kinachotoa mafunzo ya ubaharia hapa nchini na chuo kinachotambulika Kitaifa na Kimataifa pia serikali imeweza kukiwezesha chuo hicho kupata mitambo ya kisasa kama vile Full mission engine room and bridge simulator, GMDSS Simulator, High Voltage simulator, leth Mashine na Drilling mashine.
Social Plugin