Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DIWANI WA ACT WAZALENDO, WANACHAMA WENZAKE WAHAMIA CCM MCHOTEKA


Seif Hassan Dauda akizungumza na wananchi wa Kata ya Mchoteka baada ya kupokelewa na Chama cha Mapinduzi CCM akitokea ACT-Wazalendo
Wananchi na Wanachama waliojitokeza katika Mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Mchoteka Wilayani Tunduru
Wananchi na Wanachama waliojitokeza katika Mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Mchoteka Wilayani Tunduru

Na Regina Ndumbaro - Tunduru.

Katika mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Mchoteka, Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, wananchi wamejitokeza kwa wingi kushiriki sherehe za kumkaribisha rasmi Diwani wa kata hiyo, Seif Hassan Dauda, aliyerudi CCM akitokea ACT-Wazalendo. 

Tukio hilo kubwa limeongozwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali, likiwa ni ishara ya kuungwa mkono kwa kasi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Katika mkutano huo, CCM imepokea wanachama wapya 121 kutoka ACT-Wazalendo, ikiwa ni pamoja na viongozi muhimu kama Katibu wa ACT Wazalendo kata ya Marumba ndugu Athuman Mtalika almaarufu Kasopola na Katibu wa vijana wa ACT kata ya Mchoteka. 

Uhamiaji huu mkubwa umeonyesha wazi kuimarika kwa imani ya wananchi kwa sera na utekelezaji wa ilani ya CCM katika maeneo yao.

Wananchi hao wameeleza wazi kuwa sababu kuu ya kurejea CCM ni kuridhishwa na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo chini ya serikali ya Dkt. Samia. 

Miongoni mwa mafanikio hayo ni ukarabati mkubwa wa kituo cha afya Mchoteka, upatikanaji wa gari la wagonjwa kwa kituo hicho, ujenzi wa mabweni ya shule ya sekondari ya Mchoteka, pamoja na ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Likweso.

 Aidha, miradi mikubwa ya maji inayohudumia kata za Marumba na Mchoteka kwa pamoja, upatikanaji wa umeme katika kata nzima, pamoja na barabara zinazopitika kwa urahisi zimeongeza matumaini na faraja kwa wananchi.

Kwa pamoja, wamesema kuwa hawana cha kumlipa Rais Dkt. Samia zaidi ya kuhamia na kuunga mkono CCM, kama ishara ya kuthamini jitihada na maendeleo yanayoendelea kuwaletea tija katika maisha yao ya kila siku.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com