Wananchi wa Mtaa wa Mahina Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu wakishuhudia Kondoo waliouawa na Fisi.
Na Derick Milton, Bariadi.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida Kundi Fisi limevamia nyumbani kwa Mageni Maduhu mtaa wa Mahina kata ya Somanda Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu na kushambulia na kuwaua Kondoo wake 21
Tukio hilo limetokea jana April Mosi, 2025 majira ya saa nne usiku, ambapo fisi hao walivamia kwenye zizi la kondoo hao na kuwashambulia wote.
Mageni Maduhu akisimulia tukio hilo amesema kuwa lianza kusikia mlio wa fisi mmoja majira hayo ya usiku, akatoka nje na kuanza kumkimbiza.
Anasema baada ya kumkimbiza fisi huyo njiani alikutana na kundi jingine la Fisi ndipo alipoamua kurudi nyumbani na alipoelekea kwenye zizi la kondoo alikuta damu nyingi na kondoo wake wote wakiwa wamekufa.
“ Kwenye zizi kulikuwemo na Kondoo 30, ambao wameshambuliwa hadi kufa ni 21 na kondoo wengine 9 hatuwaoni walipo mpaka sasa, Kondoo wengine walikuwa na mimba na wameuawa, fisi walikuwa wengi sana,” amesema Maduhu.
Mwenyekiti wa Mtaa huo Mangu Mangolyo akizungumzia tukio hilo amesema kuwa limekuwa tukio la kushangaza kwani halijawahi kusikika au kuona fisi wanashambulia au kula kondoo wengi kiasi hicho.
Magonlyo amesema kuwa alifika kwenye tukio hilo na kukuta kweli Kondoo wote wameshambuliwa na kuuawa, ambapo alieleza tukio hilo linashangaza kwani fisi huwa hawana utaratibu wa kushambulia kondoo wengi kiasi hicho.
Mkuu wa Wilaya hiyo Simon Simalenga ambaye alifika kwa ajili ya kushuhudia tukio hilo alisema kuwa mpaka sasa bado wanaendelea na uchunguzi wa kubaini kama ni kweli fisi ndiyo wametenda tukio hilo au hapana.
Simalenga alitoa pole kwa familia ambayo imekubwa na tukio hilo, ambapo alieleza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vimeanza uchunguzi wa tukio hilo ikiwemo mamlaka ya wanyamapori Tanzania.
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya ametangaza kuanza rasmi kwa msako wa Fisi katika maeneo yote yenye vichaka kwenye Halmashauri ya Mji wa Bariadi, ambapo alieleza wameanza kupata taarifa za uwepo wa wanyama hao.
“ Kwa tukio hili lazima tufanye msako mkali wa kupambana na wanyama hawa, tutafanya msako kwenye maeneo yote, maana tumeanza kusikia na kuona uwepo wa hao wanyama kwenye halamshauri ya mji wa Bariadi,” amesema Simalenga.
Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya amewatahadharisha wananchi wote ambao wanadaiwa kufuga wanyama hao kuacha mara moja kwani msako huo utafanyika pia kwa watu wote ambao wanadaiwa kumiliki fisi.
“ Katika operesheni hii niwatahadharishe wale wote ambao wanamiliki fisi kwa kuwafuga wajisalimishe mara moja, tutachukua hatua kali kwa wanaofanya hivyo, “ amesema Simalenga.
Social Plugin