Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAJUMBE CCM SHINYANGA MJINI WATEMBELEA BUNGE KWA MWALIKO WA KATAMBI

 
Imeandaliwa na Marco Maduhu

MBUNGE wa Jimbo la Shinyanga Mjini, ambaye pia ni Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu)Patrobasi Katambi, amewaalika wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, kushuhudia vikao vya Bunge la Bajeti vinavyoendelea jijini Dodoma.

Wajumbe hao wapatao 100, wakiambatana na watumishi 50 kutoka Manispaa ya Shinyanga, waliwasili bungeni leo, Aprili 15, 2025, kwa lengo la kujifunza na kushuhudia kwa karibu namna shughuli za kibunge zinavyoendeshwa, hususan mijadala ya bajeti ya Serikali.

Katambi amesema kuwa mwaliko huo ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha viongozi wa chama na serikali katika ngazi ya wilaya kuwa na uelewa mpana kuhusu mchakato wa uandaaji na upitishaji wa bajeti, ili waweze kushiriki kikamilifu katika kupanga na kusimamia maendeleo ya wananchi.

“Ni muhimu kwa viongozi wetu wa chama na watendaji wa halmashauri kuelewa kwa undani jinsi Serikali inavyopanga na kutumia rasilimali za umma. Ushuhuda wao wa moja kwa moja hapa bungeni utawajengea uwezo wa kuhamasisha na kuelekeza maendeleo kwa tija zaidi,” amesema Katambi.

Ziara hiyo pia imelenga kuimarisha ushirikiano baina ya uongozi wa chama, Serikali na Bunge, sambamba na kutoa fursa kwa wajumbe hao kuelewa zaidi namna majukumu ya wabunge na Serikali yanavyotekelezwa kwa pamoja.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com